Saturday, October 6, 2012

Vita ya Sumaye, Lowassa leo - CCM wasubiri kusikia mpambano wao


WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, leo anatarajia kufanya kile alichoahidi mara baada ya kuangushwa na Dk. Mary Nagu katika uchaguzi wa kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) ya CCM, kupitia Wilaya ya Hanang.
Habari kutoka kwa watu wa karibu na Sumaye, zilisema kuwa Waziri Mkuu huyo wa zamani anatarajia kuzungumza na vyombo vya habari katika Hoteli ya Court Yard jijini Dar es Salaam leo, kuanzia majira ya saa sita mchana.
Kwa mujibu wa habari hizo, Sumaye amepanga kueleza mwenendo mzima wa uchaguzi huo na jinsi Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa alivyoingiza mkono na kusababisha aangukie pua.
Alipoulizwa nini hasa anataka kusema, Sumaye alisema: “Ukiweza kuja, utasikia mwenyewe nitakachozungumza.”
Ingawa hakuna aliyeweza kutoboa siri ya nini Sumaye anataka kuwaeleza Watanzania, lakini ni dhahiri kwamba ameamua kujifunga bomu na kujilipua kwa kueleza kile anachoamini njama za kummaliza kisiasa anazodai kufanyiwa na Lowassa.
Siku chache zilizopita mara baada ya kushindwa kwenye uchaguzi wa NEC, Sumaye alimtangazia vita Lowassa.
Sumaye ambaye hajatangaza rasmi kuwania kiti cha urais, anatarajiwa kupasua jipu leo kueleza kilichotokea Hanang na msimamo wake, na kwamba yuko tayari kuwania urais mwaka 2015 endapo Lowassa atajitosa.
Sumaye aliangushwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Nagu, katika kuwania nafasi ya ujumbe wa NEC wilaya ya Hanang, matokeo ambayo anaamini yana mkono wa Lowassa.
Pamoja na Sumaye kushindwa na Dk. Nagu kwa zaidi ya kura 167, amepokea matokeo hayo kwa shingo upande kwa kile alichoeleza kuwa ushindi huo ni wa mafisadi.
Inaelezwa kwamba tayari mwanasiasa huyo amefanya mazungumzo na baadhi ya wanasiasa wenye ushawishi wanaojipambanua kama wapiganaji wa ufisadi ili kuunganisha nguvu kwa ajili ya kukabiliana na kambi ya Lowassa.
Mbali ya kundi la Sumaye na wanasiasa wengine kuanza mkakati huo, wapo pia wanasiasa wenye majina makubwa ndani ya chama, serikali na wastaafu wanaotajwa kuingia kwenye muungano huo.
Akijibu tuhuma hizo kwa kifupi, Lowassa alisema endapo Sumaye ataitisha mkutano na waandishi wa habari na kutoa tuhuma hizo, nitajibu.
Hata hivyo, baadhi ya wafuasi wa Sumaye na watendaji wa ndani ya serikali wamesema kuanguka kwa mwanasiasa huyo mkongwe katika uchaguzi wa wilaya kunamuweka vizuri zaidi kisiasa kutokana na mazingira tete ya kisiasa ndani ya CCM, chama ambacho kimechokwa na umma.
Uchaguzi huo ulifanyika siku chache baada ya CCM kupitisha majina ya walioomba nafasi hizo huku wanachama wengi wakienguliwa kutokana na kukosa sifa katika kikao kilichomalizika mjini Dodoma hivi karibuni.
Wakati Sumaye akijipanga kupasua jipu leo, CCM kwa upande wake inasubiri kwa hamu kumsikia atakachosema.
Tangu Sumaye alipodokeza kwamba atazungumza na waandishi na kupasua jipu, baadhi ya viongozi wa CCM wamekuwa wakifuatilia kwa makini siku atakayozungumza na waandishi.
Sumaye na Lowassa wanatajwa kuwa miongoni mwa makada wanaofikiria kutaka kuwania urais mwaka 2015.

No comments:

Post a Comment