|
WAKAZI wa Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi, wametaka katiba
mpya ijayo, madaraka ya rais wa nchi ya kuteua watendaji wakuu
yaangaliwe upya na ikiwezekana yapunguzwe.
Wakitoa maoni yao juzi katika mdahalo wa katiba mpya ulioendeshwa na
Mtandao wa asasi za kiraia Mkoa wa Lindi (Lango), wakazi hao
walilishukuru shirika hilo kuwapa nafasi hiyo ya kutoa maoni kutokana na
kuikosa wakati tume ya kukusanya maoni ilipopita mkoani humo hivi
karibuni.
Mmoja wa wakazi hao, Mawazo Hashimu mkazi wa Nachingea, alisema kuwa
katika katiba ijayo, iko haja ya rais kupunguziwa madaraka ya kuwateua
watendaji na kuwepo na ukomo wa madaraka.
“Rais asiwateue wabunge kuwa mawaziri, kwani hao ni watetezi wa
wananchi na wawakilishi wao bungeni… sasa rais atakapowateua kuwa
mawaziri hawatapata muda wa kuwatetea wale waliowachagua,” alisema.
Aidha, wananchi hao walipendekeza kuwepo na ukomo wa madaraka ya viongozi kwani wamekuwa wakiongoza nchi kwa miaka 30 hadi 40.
Wananchi hao waliongeza kuwa katiba hiyo iwabane wabunge kuishi
majimboni kwao kama ilivyo kwa madiwani badala ya sasa ambapo wengi wao
wamekimbia majimboni na kuhamia jijini Dar es Salaam.
|
No comments:
Post a Comment