|
KULIKUWA na maadui watatu wa Watanzania, yaani Umasikini, Njaa na Ujinga wakati wa Uhuru mwaka 1961.
Siku za hivi karibuni wameongezeka maadui wengine, ikiwamo CCM na ufisadi, ambao nao wote hawaitakii mema Tanzania.
Cha kushangaza tunataka kuongeza adui mwingine wa kuzuia mabadiliko
katika nchi kwa sababu ya utumwa wa CCM tunazalisha adui mwingine
anaitwa V4C.
Kwanini Vision for Change idhaniwe kuwa ni utumwa wa CCM?. Yawezekana kuna majibu mengi lakini haya yanaweza kuwa mojawapo.
Kwa kuwa adui mkubwa wa CCM na serikali yake kwa sasa ni Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), na kwa kuwa CCM na vyombo vyote vya
dola vimekuwa vikiilinda CCM na kushambulia CHADEMA, na kwa kuwa CUF
nayo ili waweze kufanikiwa wameamua kuanza na mrengo huo huo wa
kujihusisha na CCM zaidi ili kushambulia CHADEMA, hakuhitajiki nguvu
nyingi mtu kufikiri kuwa Chama hiki ambacho kimekuwa kikituhumiwa kuwa
ni ‘CCM B’ kuwa kimetumwa kukandamiza nguvu ya mabadiliko inayohitajika
kukomboa watanzania.
Pengine tunapoandika kuhusu V4C Vision for Change, inawezekana
tunaonekana tunakionea wivu CUF, na dira yake ya mabadiliko
inayokataza mawazo mapya hata ndani ya Chama chenyewe.
Maana wangalipenda mabadiliko wasingekataa hoja za kundi la Hamadi
Rashidi, Shoka na Doyo waliohoji kuhusu mamlaka ya Katibu Mkuu kuwa
sehemu ya serikali.
Kutokana na athari hiyo ya Katibu Mkuu kuwa sehemu ya serikali
kumeendelea kudumaza CUF na katu kwa utaratibu huo CUF imekosa sifa ya
kuwa Chama cha Upinzani. Maana ili Maalim Seif aseme ni lazima kila kitu
kiratibiwe na Usalama wa Taifa, ili asafiri ni lazima safari yake
iratibiwe, ili anywe au ale au kuvaa masuala hayo lazima yahusishe watu
wa usalama. Hivyo hata maneno au sera wanazopanga akiwa CUF zinafika CCM
kwanza kwa kupitia watu wa usalama, na hivyo CCM waweza kujihami na
sera za CUF au kuzitekeleza haraka zaidi kabla hazijaleta madhara kwa
serikali. Kwa utaratibu huu Chama hiki kitakuwa cha upinzani lini?
Ukiachilia mbali Vision for Change, inayosadikiwa kuwa ni utumwa wa
CCM, hata huko nyuma CUF haijaweza kuwa na operesheni yenye mafanikio.
Vision for change ni mkakati tu kati ya mikakati mingi iliyobuniwa
kudhoofisha upinzani nchini, ndio maana Vision for Change imeamua
kuanzia Arusha na kujitapa kuwa inaweka kambi ya kudumu, mahali ambapo
kuna chama kiingine maarufu cha Upinzani. CHADEMA Arusha kina madiwani
na mbunge alikuwepo japo ana kesi. Mwenyekiti wa CUF aliamua kuanzia
huko ambako Upinzani umekomaa akaacha Tabora kwao ambapo hawajawahi kuwa
hata na diwani wa chama chake tangu aukwae uenyekiti wa kudumu na
ugombea wa kudumu kupitia chama chake, kana kwamba wengine hawawezi.
Mwaka 1999, chama hiki kiliasisi kitu kilichoitwa “Mfuko wa
Mwenyekiti”, kwa lengo la kukusanya pesa kusaidia kampeni za Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2000. Mfuko huo ulikuwa chini ya Uenyekiti wa Ania
Chaurembo na Katibu wa Mfuko huo alikuwa Kinga Ally Shamte ambaye kwa
sasa ametimkia CCM. Hadi leo makala hii inaposomwa, CUF hawajawahi
kutangaza kuwa zilipatikana shilingi ngapi, au zilitumikaje kwa kuwa
zililenga kusaidia mambo ya Kampeni.
Mwenyekiti wa chama anayesifiwa kuwa profesa wa uchumi, asiyeleta
mapato na matumizi huyu ana sadifu kwa tabia iliyopo kwa chama tawala.
Kama hiyo haitoshi mwaka 2006 kupitia kikao cha baraza kuu CUF
ilikubali kuwa watatenga milioni thelathini (30,000,000) kutoka ruzuku
ya serkali ambayo wakati huo chama hicho kilikuwa kinapokea
177,000,000/-. kiasi cha milioni 30 kilitengwwa mfululizo kila mwezi kwa
miaka mitano lakini baada ya kikao cha Kamati Kuu 2010 kuelekea kwenye
Uchaguzi Mkuu mshituko ulikuwa mkubwa baada ya chama hicho kuonekana
hakina pesa zinazokadiriwa kuwa bilioni moja na nusu. Ndani ya utaratibu
mbovu huu ni watanzania wangapi wapo tayari kuchangia pesa kwa chama
kilichopoteza mapesa lukuki hadi sasa hakina hata magari ya ofisi?
Iinafaa CUF wanapokuja kwa wananchi wawaeleze operesheni zingine au
sera zingine walizoanzisha zikiwemo ngangari na Ngunguri kinoma, au
Zinduka iliyoasisiwa baada ya Chama kiingine kuanzisha operesheni
sangara, waeleze kwanini zilishindwa? au zilikuwa na mafanikio kiasi
gani? Kwanini walichangisha pesa wakati wa uchaguzi zikakosekana? Pesa
za sasa wanazochangisha kila mbunge zaidi ya milioni mbili, na kila
mwakilishi shilingi laki 6 zinatumikaje katika chama.
Kama utamaduni wa kula michango haujadhibitiwa, waliofuja michango
ndio hao hao wanaosimamia wazo la Vision for Change, je dira hii ya sasa
itafanikiwa? wamebadilisha mfumo wa kudhibiti pesa?
Kama katika chama, Naibu katibu Mkuu anashindwa kueleza ‘imprest’ ya
128,000,000, Shaweji Mketo naye akashindwa kuelezea matumizi ya sh
milioni 81, huku Maole naye akishindwa kutolea maelezo ya sh milioni 6.
Ni dalili za wazi kabisa kuwa pesa za Chama zinagawanywa, na wanaogawana
ndio wanaimba nyimbo za kumsifu Katibu Mkuu, na Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar ambaye anaruhusu matumizi holela ya pesa za chama
kinachoongozwa na profesa wa uchumi, kisicholeta mapato na matumizi.
Kwa utaratibu huu watanzania tuache kuuliza pesa tunazochangia
zimekwenda wapi? tutaache kuuliza kwanini chama chetu hiki hakinunui
magari hata angalau gari ya Mwenyekiti wa chama, ukiacha ile iliyotolewa
kwa njia ya manunuzi ya kirafiki na mwakilishi mmoja toka Zanzibar .
Huu ndio uendeshaji wa chama kinachotaka tuwachangie?
Kama kwa nyakati zote wamechangiwa pesa lukuki hawakufanyia kazi za
Chama. hizi za sasa zimetoka wapi? na Je operesheni hii itakuwa
endelevu? mbona wenyewe wanaruhusiwa kufanya maandamano na wengine
wanakatazwa?
Akilihutubia taifa katika hotuba yake ya kila mwezi, Ikulu mwezi
Februari, Rais Kikwete alisema kufanya maandamano na mikutano ni haki ya
msingi ya vyama vya siasa na raia.
Lakini, kuigeuza fursa hiyo kuwa ni jukwaa la kuchochea ghasia na kwa
nia ya kuiondoa serikali iliyoko madarakani kwa mabavu ni matumizi
mabaya ya fursa hiyo. (jambo ambalo linafafanuliwa kuwa ni uhaini)
Kikwete alisema "Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila miaka mitano
tunafanya uchaguzi wa kuchagua viongozi wetu. Uchaguzi wa mwisho
tumefanya Oktoba 31, 2010. Kabla ya hapo tulikuwa na kampeni
zilizochukua karibu miezi mwili na nusu. Kila chama kilielezea jinsi
kitakavyokabiliana na matatizo yanayowakabili wananchi wa nchi yetu
ikiwa ni pamoja na haya wanayoyazungumza sasa.
Wiki hiyo hiyo gazeti la serikali la Daily News lilimkariri Msajili wa
Vyama vya Siasa, John Tendwa, akisema kauli zinazotolewa kwenye
maandamano ya CHADEMA za kumpa muda wa siku tisa Rais Kikwete kutekeleza
mahitaji yao ni za kichochezi na zinaweza kuingizwa katika makosa ya
uhaini kwa kuwa kinawachochea wananchi waichukie serikali yao.
Nimetafakari sana kauli za viongozi hao, na kujiuliza kama kweli
wanachukizwa na uhaini kwanini wao wanazungumzia uhaini kama kuna
mikutano ya CHADEMA tu?
Nimeshangazwa na kauli za hivi karibuni za viongozi wa Chama cha
Wananchi (CUF) kuwa “mchagueni Lipumba aende Ikulu”, “mchagueni Lipumba
aende Magogoni.” Hizi ni kauli za kila siku zinazotajwa na viongozi wa
CUF, katika hiki kinachoonekana kuwa ni Vision for Change.
Viongozi wetu wa kitaifa, hasa wale wasiopenda vyama vyenye nguvu hasa
kinachounda kambi ya upinzani wangesikia hayo tungesikia sauti kama
hizo hapo juu, kuwa Wameanza kampeni, ni wahaini, hawataki nchi
itawalike, wanasumbua wananchi. Lakini kwa sasa kwa sababu Chama
kinachofanya hayo ni kipenzi cha serikali, ni CCM B, basi hata serikali
imekaa kimya kwa masuala mbalimbali yanayofanywa na CUF, na CUF kwa
kutumia mwanya wa kupendelewa na serikali inaendelea kutangaza mambo
yale yale, hadharani, bila kificho. Tena wakiwa na akili timamu.
Rais aliyepo madarakani ni Jakaya Mrisho Kikwete, iwe alichaguliwa
kihalali au hakuchaguliwa kihalali ila ndiye aliyeapishwa kwa katiba
iliyopo. Rais hajafa. Ni mzima, hajaugua kiasi cha kushindwa kutekeleza
kazi za kawaida. Lakini chama kiingine kinaendelea na Kampeni za kunadi
mgombea. Chama cha CUF kilifanya vile tarehe 6, Januari 2012 katika
Viwanja vya Bakhresa, Manzese jijini Dar es Salaam.
Chama hicho kikarudia yale yale Jangwani katika mkutano wa Vision
for Change (Dira ya mabadiliko). Kauli hiyo hiyo imeendelea kurudiwa
rudiwa Arusha.
Lakini katika hayo yote, serikali ipo kimya, kwa kuwa anayefanya hayo
ni sehemu ya serikali, ni sehemu ya chama tawala, ni kipenzi chao.
Kampeni hii ni kwa faida ya nani? Na kwanini serikali ipo kimya.
Utaachaje kusema hii ndiyo CCM “B”.
Tume ya Uchaguzi haijatangaza kampeni, nina hakika huu si wakati wa
kampeni za kutangaza wagombea, bahati mbaya sana hata katiba ya CUF kama
ipo sitegemei kama inaruhusu ‘ujinga wa aina hii’ yaani wa kidikteta,
wa kujitangazia mgombea nje ya taratibu za Chama.
Vikao vya kupitisha wagombea CUF kilifanyika lini? Kama hakikufanyika
imekuwaje Prof. Ibrahim Lipumba, anayeonekana kuwa ni msomi, anayeelewa
kilichopo katika katiba yao akakubali kutawazwa kuwa mgombea wa kudumu
wa CUF bila kufuata utaratibu?. Huu ni Unyimifu au ubinyifu wa
demokrasia.
Kutokana na tabia hii huenda ndio maana hawakukubali mabadiliko ya
uongozi yaliyokuwa yakiongozwa na Hamad Rashid Mohamed ili wao wabaki na
Vyeo siku zote. Uhalali wa kampeni za CUF kumnadi Ibrahimu Lipumba kuwa
Mgombea tunayepaswa kumuunga mkono aingie Ikulu upo wapi muda huu?
Najua watu wa CUF baadhi wana jazba wanapoona wanaandikiwa ukweli
hukimbilia katika kauli za kitoto kulaumu kuwa waandishi hawapendi CUF.
Prof. Lipumba anayeonekana kuwa msomi, anashindwaje kuona kasoro hii
kubwa ya kuwabania wengine wasijitokeze katika chama chake kuwania
nafasi hiyo badala yake anakubali kunadiwa kuwa ni mgombea nje ya
taratibu za chama chake? hayo ndiyo malengo ya V4C?
|
No comments:
Post a Comment