Sunday, October 7, 2012

Mjane wa Mwangosi achangiwa mil. 5.6/-

MJANE wa marehemu Daudi Mwangosi, Itika Mwangosi, amechangiwa kiasi cha sh milioni 5.6, zikiwa ni rambirambi za kifo cha mumewe.
Fedha hizo zimepatikana kufuatia mchango ulioendeshwa na mtandao maarufu wa kijamii nchini wa Mjengwablog, unaomilikiwa na mwanahabari nguli, Majid Mjengwa, wa mkoani Iringa, ambao ulikabidhiwa kwa mjane huyo juzi.
Waliochangia rambirambi hiyo ni pamoja na wanahabari, wanasiasa, wahaharakati na wasomi mbalimbali.
Kupitia blog yake hiyo, Mjengwa kwa niaba ya mjane huyo aliwashukuru wote waliojitolea michango hiyo ili kumwezesha kupata mtaji wa kuanzisha shughuli za kujikimu pamoja na watoto wake.
Mwangosi aliuawa Septemba 2, mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo wakati polisi walipokuwa wakiwazuia viongozi na wafuasi wa CHADEMA kufanya mkutano wao wa ndani wa kata baada ya kuzindua tawi la chama hicho kijijini hapo.
Mpaka sasa askari mmoja wa Jeshi la Polisi mwenye namba G. 2573, Pacificus Cleophase Simon (23), ameshafikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya Daudi Mwangosi.

No comments:

Post a Comment