|
WAZIRI Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, amemtaka Spika
wa Bunge, Anna Makinda, kutumia madaraka na mamlaka yake kutangaza kwa
umma kamati nyingine ya kudumu ya Bunge itakayoshughulikia masuala ya
gesi asili kabla na wakati wa mkutano wa Bunge ujao mwishoni mwa mwezi
huu.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo kupitia CHADEMA, alisema hatua
hiyo ni kutokana na hali tete na tata kuhusu sekta ndogo ya gesi asilia
nchini na kwa kuzingatia umuhimu na unyeti wa sekta hiyo katika uchumi
wa nchi na maisha ya wananchi.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mnyika alisema pamoja
na mambo mengine, Spika Makinda aelekeze kamati hiyo kupokea na kujadili
taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge ya mwaka 2011 kuhusu sekta
ndogo ya gesi asili ikiwemo juu ya hatua iliyofikiwa katika
kushughulikia tuhuma za ufisadi.
Madai mengine ni ya mapunjo ya fedha za mauzo ya gesi asili na hatua
iliyofikiwa katika maandalizi ya sera, mpango mkakati na sheria ya gesi
asili.
“Hatua hii ni muhimu kufuatia ukimya wa Waziri wa Nishati na Madini,
Prof. Sospeter Muhongo kuhusu kauli yangu ya Oktoba 4, 2012 ya kutaka
taarifa ya ufafanuzi kuhusu utafutaji wa mafuta na gesi asili nchini
iliyotolewa na wizara hiyo Septemba 21 mwaka huu ifutwe,” alisema.
Alisema kuwa taarifa hiyo ya wizara ilieleza kuwa maandalizi ya sera
ya gesi asili yapo katika hatua za mwisho wakati ambapo kamati
mbalimbali za kudumu za Bunge hazijahusishwa katika mchakato huo muhimu
pamoja na kuwa mamlaka ya kutunga sera kwa mfumo wa sasa ni ya Baraza la
Mawaziri.
“Kwa unyeti na upekee wake sera ya gesi, Spika wa Bunge anapaswa
kuwezesha Kamati za Kudumu za Bunge zihusishwe ili pawepo mashauriano na
maridhiano kwa mapana na marefu,” alisema.
Mnyika alisema izingatiwe kwamba katika mkutano wa nane wa Bunge,
Spika alitangaza kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini
imevunjwa na kwamba majukumu iliyokuwa ikishughulikiwa yatashughulikiwa
na kamati nyingine kwa mujibu wa madaraka na mamlaka ya spika.
|
No comments:
Post a Comment