Saturday, August 11, 2012

Mizinga ya JWTZ yazua hofu Dar

WAKAZI wa Kibamba, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, usiku wa kuamkia jana walilazimika kuzikimbia nyumba zao baada ya kutokea kishindo kikubwa cha milipuko katika kambi ya vifaru vya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Mloganzila.
Tukio hilo limetokea majira ya usiku kati ya saa 5 hadi 7:04 ambapo milipuko mitano ya mizinga ilisikika kutoka eneo hilo la Mlongazila katika wilaya jirani ya Kisarawe mkoani Pwani, ikiambatana na kukatika kwa umeme, mawasiliano ya simu na mvua kubwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima, wakazi hao walisema tukio hilo limewashtua kwa sababu halijawahi kutokea katika kipindi cha miaka zaidi ya saba walichoishi kwenye eneo hilo.
Walisema kuwa waliamua kukimbia na kuelekea kusikojulikana kwa lengo la kuokoa maisha yao, kwani walihofia madhara ya milipuko ya mabomu kama ilivyotokea kwenye kambi za Mbagala na Gongo la Mboto.
Mmoja wa wakazi hao, Mhando Yahaya, alisema wakazi wote wa Kibamba walikimbilia kwenye kijiji kidogo cha Kibwegele, wakiacha nyumba pamoja na mali zao bila kujali.
“Ujue serikali inabidi itowe angalizo kabla na si kufanya siri kwa kuwa matokeo yake ni kama haya, wananchi tunatishika na kukimbia hovyo usiku huu, mvua na giza vikituandama,” alisema Yahaya.
Naye Egnes Habiyu, alisema milipuko kama hiyo, imesababisha baadhi ya wagonjwa wa moyo kushtuka hadi kufikia hatua ya kuishiwa nguvu na wengine kujeruhiwa wakati wakikimbia.
Akifafanua kuhusu milipuko hiyo, Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, alisema hayo yalikuwa mazoezi ya kawaida na kwamba hayana uhusiano wowote wa kivita.
Vilevile aliwatoa wasiwasi wananchi kuwa milipuko hiyo haina madhara bali ni moja ya mazoezi ya kawaida.
Kanali Mgawe alisema taarifa zilitolewa mapema kwa wakazi wanaoishi jirani na kambi hiyo, hivyo kwa vile mazoezi yalifanyika usiku kukiwa kumetulia sauti ya milipuko hiyo ilisikika hadi mbali.

No comments:

Post a Comment