|
HELEN Kijo Bisimba, ni jina linalosikika ndani na nje ya
Tanzania. Huyu ni mama shupavu, jasiri, mpambanaji na mwanaharakati wa
kutetea haki za binadamu, ambaye ameamua kujitoa kutoa mchango wake
katika kuendeleza na kulinda ustawi wa taifa la Tanzania.
Tumezoea kusema kwamba ‘nabii hasifiki nyumbani’! Inawezekana ni hivyo
kwa mama huyu, ambaye kazi anazozifanya zinaheshimika na kusifiwa
kwenye ulingo wa kimataifa kuliko hapa nyumbani? Inawezekana ni kwa vile
kazi anayoifanya mama huyu inaigusa serikali jichoni au kwa vile
amejifunga kibwebwe kupambana na mfumo dume na kutaka kuutokomeza? Au
labda ni kwa vile bado viongozi wengi kwenye ngazi ya maamuzi katika
taifa letu ni wanaume?
Juzi, sote tumeshuhudia kwenye vyombo vya habari Dk. Bisimba akisoma
taarifa ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kuamua kuiburuza
Serikali ya Tanzania kwenye Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC)
iliyoko The Hague, Uholanzi.
Hiki ni kitendo cha ujasiri na kujitoa, maana ni wachache wanaoweza kuthubutu kufanya hivyo bila kuogopa matokeo yake.
Hata hivyo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, kinachoongozwa na
Bisimba, kimekuwa mstari wa mbele kutetea haki za watoto, wanawake na
watu wote wanaokandamizwa; kunyang’anywa ardhi yao na matuko mengine ya
kifisadi yanayoendelea katika taifa letu. Kituo hiki kimekuwa sauti ya
wanyonge.
Mama huyu amejitofautisha na baadhi ya watu wanaoongoza mashirika
yasiyo ya kiserikali (NGO’s) mbalimbali katika taifa letu la Tanzania;
hata kama NGO’s hizo zinakuwa ni za kutetea haki za binadamu, viongozi
hao wamekuwa wakifanya kazi kwa malengo ya kupata mshahara tu!
Au kwa lengo la kujenga majina yao na kujitafutia sifa. Ni tofauti
kabisa na Bisimba, ambaye Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimekuwa
sehemu ya maisha yake.
Bila unafiki na kujipendekeza, Bisimba anaonekana wazi kuguswa na kila
aina yoyote ile ya ukiukwaji haki za binadamu katika taifa letu.
Amekuwa mstari wa mbele kupinga ufisadi, rushwa na uporwaji wa
rasilimali katika taifa letu.
Ameshiriki kuipigania demokrasia na utawala bora na kilio cha katiba
mpya katika taifa letu. Haogopi kusimama na kusema wazi msimamo wake na
msimamo wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.
Yuko tayari kusema hata yale yasiyopendeza kwenye masikio ya watawala.
Mama huyu aliyezaliwa mnamo mwaka wa 1954 mkoani wa Kilimanjaro, ndiye
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
kinacholinda na kutetea haki za binadamu za kila Mtanzania na
kuhakikisha kwamba kila raia anakingwa na aina zote za udhalilishaji.
Mapenzi ya kutetea haki za binadamu na moyo wa unaharakati yalionekana
kwake kwenye miaka ya 1970 alipokuwa akisoma sekodari ya Korogwe kule
Tanga.
Alifukuzwa shule kwa muda, baada ya kukataa shinikizo la walimu wake
kuomba msamaha kwa barua ya kudhalilisha aliyoandikiwa mwalimu mkuu wa
shule. Alikataa kuomba msamaha wa kosa ambalo yeye hakutenda.
Kwa vile alikuwa msaidizi wa kiranja wa shule alikubali kufukuzwa
kuliko kuomba msamaha. Baba yake mzazi alikwenda kumwombea msamaha,
lakini walimu walikataa. Hadi alipoamua baadaye kuzungumza na walimu na
hatimaye kuomba msamaha kwa kosa ambalo hakulitenda mwenyewe.
Tukio hili lilimjengea moyo wa ujasiri ambao hadi leo hii zaidi ya
miaka 40, amekuwa akitetea haki za wanyonge, wanaume kwa wanawake,
vijana kwa wazee.
Mama huyu, alikuwa kati ya watu wa kwanza kumshughulikia Dk. Stephen Ulimboka alipotekwa, kupigwa na kuteswa.
Kila mtu alishangaa jinsi mama huyu alivyopata habari haraka juu ya
tukio hilo la kinyama na kufanya haraka kushiriki kutoa msaada kwa Dk.
Ulimboka.
Alimsaidia kumfikisha hospitali na kuendelea kuishinikiza serikali
ifanye uchunguzi wa kina kubaini watu waliofanya unyama huo.
Wakati wa mgomo wa madaktari, sauti ya Bisimba ilisikika kote kwenye
vyombo vya habari. Yeye na wanaharakati wengine waliishinikiza serikali
kufanya haraka kuumaliza ili kunusuru uhai wa raia wasiokuwa na hatia.
Na katika hali isiyokuwa ya kawaida mama huyu na wanaharakati wengine
walikamatwa na polisi na kuhojiwa wakati walipofika Muhimbili, kutaka
kujua kinachoendelea.
Mwaka 2001, alikuwa mwanamke mwanaharakati wa kwanza kupinga na
kulaani mauaji yaliyotokea Zanzibar. Kitendo hicho kilimletea sifa ndani
na nje ya Tanzania.
Mwaka 2008 alikuwa mwanamke wa kwanza kupokea tuzo ya Mwanamke Jasiri inayotolewa na Balozi wa Amerika nchini Tanzania.
Mama huyu amekuwa mstari wa mbele kupinga hukumu ya kifo. Siku ya
Kupinga Hukumu ya Kifo inaangukia siku yake ya kuzaliwa ambayo ni Oktoba
10, hivyo mwaka huu anapoadhimisha miaka 58 ya kuzaliwa, ana imani
kubwa kwamba iko siku adhabu hii ya kifo itakuja kufutwa nchini
Tanzania.
Mama huyu ni kati ya watu wanaotamani kuona Tanzania inawaruhusu
wasichana wanaopata mimba wakiwa shuleni kuendelea na masomo, na elimu
ya kujitambua inafundishwa shuleni.
Kwa maoni yake, wakati mwingine wasichana wanapachikwa mimba kwa kuwa
na uelewa mdogo juu ya kujamiana; na kwamba wazazi wasione aibu kuongea
na watoto wao juu ya suala la kujitambua na mahusiano, maana ukimya
katika hili ni hatari zaidi kuliko faida.
Mama huyu yuko mstari wa mbele kupinga vifo vya wanawake wakati wa
kujifungua na vifo vya watoto wadogo. Ameunga mkono na kushiriki kampeni
zote zinazoendelea za kupambana kupunguza vifo vya wajawazito.
Pia kwa kupitia Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu anaongoza kampeni
ya kutokomeza ukeketaji, kuwarithi wajane na aina nyingine ya
unyanyasaji kwa wanawake.
Mama huyu alianza kukiongoza Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
mwaka 1996, na ni mmoja wa waanzilishi wa kituo hiki cha kutetea na
kulinda haki za binadamu.
Ni mjane tangu mwaka 1994. Ana watoto wanne, wawili ni mainjinia,
mmoja ni daktari na mwingine ni mhasibu. Lakini pia anatunza watoto
yatima nyumbani kwake na ni mwanachama wa wanawake wajane katika kanisa
anapoabudu.
Mbali na kuwatunza watoto yatima nyumbani kwake, yeye amekuwa sauti ya watoto wanaojilea na kujitunza.
Wakati kuna watafiti wanaopinga Tanzania kuwa na familia za watoto
wanaojilea wenyewe na kujitunza, Bisimba anaamini kwamba Makete na
Karagwe, alikofanyia utafiti wa tasinifu yake ya shahada ya uzamifu,
kuna familia za watoto wanaojilea na kujitunza kutokana na janga la
ugonjwa wa ukimwi.
Mwaka 2008 mpaka 2001, alichukua likizo ya masomo na kwenda Uingereza
kuchukua shahada ya uzamifu kwenye sheria na haki za binadamu.
Tasinifu yake ulikuwa ni utafiti juu ya haki za watoto. Alitaka sauti
ya watoto wa Afrika isikike, alitaka kujua jinsi watoto wanavyouelewa
mfumo wa serikali. Anaamini kwamba kwa kuelewa mawazo ya watoto,
serikali yoyote inaweza kutenda vizuri siku zinazokuja, maana watoto wa
leo ndio viongozi wa kesho.
Kabla ya kujiunga na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, mama huyu
alikuwa mwalimu wa Kiingereza na Kiswahili katika Taasisi ya Elimu ya
Watu Wazima alikofanya kazi kwa kipindi cha miaka 10.
Marehemu mume wake ndiye aliyemshauri kusomea sheria. Wakati
anajiunga na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, alikuwa bado
anafundisha taasisi na kujitolea kwenye Shirika la WILDAF (Women in Law
and Development in Africa) ambalo aliliwakilisha kwenye mkutano wa
wanawake wa Beijing mwaka 1995.
Mama huyu ni kiongozi wa mfano. Hata wafanyakazi wenzake wanampenda na
kumheshimu. Wengi amewaambukiza roho ya kutetea haki za binadamu na
ujasiri wa kusimama kidete mbele ya haki.
Ukifika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, unakutana na mkurugenzi
ambaye licha ya kuwa kiongozi wa kituo hicho, ni mama mwenye sifa zote
za umama; kulea, kuelekeza, kujali, kutokuwa na uroho wa elimu,
kuwashughulikia wengine, kuguswa na matatizo ya wengine na kuambukiza
roho ya ujasiri kwa wafanyakazi wenzake.
Mama huyu pamoja na kazi kubwa alizonazo za kukiongoza kituo, bado ana
nafasi ya kuihudumia familia yake, kuangalia mpira na watoto na wajukuu
zake na pia kupata nafasi ya kuimba kwenye kwaya ya kanisa.
Huyo ndiye Bisimba, mwanamke shujaa, jasiri, msomi, mzalendo, mwanaharakati na mtetezi wa haki za binadamu.
|
No comments:
Post a Comment