KAMATI iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel
Nchimbi, kuchunguza mauaji ya mwanahabari, Daudi Mwangosi, imekamilisha
kazi yake, huku ikitoa siri nzito.
Siri hiyo ambayo huenda ikasababisha baadhi ya vigogo wa polisi
kupoteza kazi, itawekwa hadharani katika mkutano wa waandishi wa habari
Jumanne ijayo, mbele ya kamati hiyo na Waziri Nchimbi mwenyewe.
Tayari kamati hiyo iliyofanya kazi kwa siku 30, imekabidhi ripoti yake
kwa Dk. Nchimbi jana, kumpa fursa ya kuipitia kabla ya ukweli kuhusu
mauaji hayo kuwekwa hadharani.
Ripoti hiyo ilikabidhiwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Theophil
Makunga ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Mwananchi Communication.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Makunga alisema kamati yake ilifanya ziara
mkoani Iringa na kufanya mahojiano na wadau mbalimbali mkoani humo na
jijini Dar es Salaam.
Mara baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo jana, Dk. Nchimbi kupitia
taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari, ameahidi kuwa yeye pamoja
na kamati hiyo, watafanya kikao na waandishi wa habari kueleza
kilichobainishwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Msemaji wa Wizara hiyo,
Isaac Nantanga, Nchimbi mbali na kupokea ripoti hiyo aliishukuru kamati
kwa kazi waliyoifanya.
Ripoti ya kamati hiyo imekabidhiwa ikiwa ni takribani zaidi ya mwezi
mmoja tangu mwanahabari huyo alipouawa kinyama na polisi Septemba 2,
mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi wakati polisi
walipovamia na kutawanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) waliokuwa wakifungua tawi la chama hicho katika kijiji hicho.
Mazingira ya kifo cha Mwangosi yamesababisha uhasama mkubwa baina ya
Jeshi la Polisi na wanahabari ambao katika baadhi ya mikoa wameamua
kususia kazi za jeshi hilo.
Mgogoro huo ulisababisha Nchimbi afikie hatua ya kuunda kamati hiyo
baada ya siku tatu tangu kutokea kwa mauaji hayo ili kubaini utata wa
kifo hicho.
Kamati hiyo yenye watu watano iliwashirikisha Jaji Mstaafu wa Mahakama
Kuu, Steven Ihema, Makunga na Ofisa wa Baraza la Habari Tanzania (MCT),
Pili Mtambalike.
Wengine ni mtaalamu milipuko kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), Kanali Wema Wapo pamoja na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi,
Isaya Mungulu.
Dk. Nchimbi aliiagiza kamati hiyo kufanya kazi yake kwa siku 30 na
kukabidhi ripoti kwake na kueleza umma chanzo cha tukio hilo.
Kamati hiyo ilipewa hadidu za rejea sita huku Nchimbi akiahidi kwamba
askari watakaobainika kuhusika na tukio hilo, watachukuliwa hatua za
kinidhamu.
Hadidu za rejea ni pamoja na maswali kadhaa kuhusu chanzo cha kifo cha Mwangosi.
Nyingine ni ile inayotokana na kuwepo kwa taarifa kwamba kuna uhasama
kati ya Jeshi la Polisi na waandishi wa habari wa Mkoa wa Iringa na
kama kuna waandishi watatu wa habari wanatafutwa na polisi.
Hadidu nyingine ni kujibu maswali kama nguvu iliyotumika katika
kukabiliana na tukio lile ilikuwa kubwa kupita kiasi na je, kuna
taratibu za kukata rufaa kwa chama kinachodhani hakikutendewa haki na
Jeshi la Polisi?
Pia aliiagiza kamati hiyo ichunguze kama kuna tatizo kwa vyama vya siasa kwamba, havina mahusiano mazuri na Jeshi la Polisi.
Hata baada ya kamati hiyo kuundwa, waandishi wa habari katika baadhi
ya mikoa, ikiwamo Dar es Salaam waliongoza maandamano ya kulaani mauaji
ya mwanahabari mwenzao.
mwalimu mwakalindile
No comments:
Post a Comment