|
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake (UWT) CCM mkoani Dar es Salaam,
Zarina Madabida, aliyekuwa akitetea kiti chake, ameanguka na nafasi yake
kuchukuliwa na Janeth Masaburi, Mke wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam,
Didas Masaburi.
Wakati Mama Madabida akianguka, vurugu kubwa zimeibuka katika uchaguzi
mwingine wa CCM uliofanyika jana katika viwanja vya Karimjee baada ya
wapambe wa wagombea wawili wanaowania nafasi ya Baraza Kuu na Mkutano
Mkuu Taifa kuchapana makonde hadharani.
Zarina ambaye anakuwa mwenyekiti mpya wa umoja huo mkoani Dar es
Salaam, aliibuka na ushindi wa kura 168 dhidi ya 140 za Mama Madabida,
huku Irine Makinda akiambulia kura tatu tu.
Uchaguzi huo uliotawaliwa na vituko, vijembe na kejeli za aina yake
kutoka kwa wafuasi wa pande hizo mbili, ulifanyika jana katika viwanja
vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Awali kabla ya matokeo hayo kutangazwa baadhi ya wajumbe waliangua
vilio kupinga ushindi wa Mama Masaburi, huku waliounga mkono hata kabla
ya msimamizi wa uchaguzi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mecky Sadick
kutangaza matokeo, walikuwa wakiimba na kucheza kushangilia ushindi.
Shangwe, nderemo na nyimbo za taarab zilianza kusikika hata kabla na
baada ya mshindi kutangazwa huku wajumbe wengine wakirusha maneno na
kudai kuwa salamu zimfikie Sophia Simba ambaye ni Mwenyekiti wa UWT
Taifa anayetetea kiti chake.
Hata hivyo baada ya kutangazwa mshindi baadhi ya wajumbe wa uchaguzi
huo walipiga vijembe na kudai kuwa watu wanaotaka kuiongoza CCM kama
chama chao ujumbe uwafikie kwani wajumbe wa sasa sio wa zamani.
“Habari ndio hiyo na iwe chachu ya mabadiliko kwa CCM na wakae wakijua
kuwa CCM ya zamani sio ya sasa, walifanya chama kama chao sasa ni
mabadiliko tu,” ilisikika sauti ya mmoja wa wajumbe wa uchaguzi huo.
Naye Katibu wa UWT tawi la Kimara, Royita Phares, alisema
kilichosababisha anguko la Mama Madabida ni hatua yake ya kuingilia
uchaguzi wa wilaya.
Naye, Mama Madabida alisema kama wanachama wakizungumza kupitia kura
zao, mambo yanakuwa yameisha na kinachofuata ni kujenga jumuiya imara na
kutoruhusu kukatika vipande.
Mwenyekiti mpya mama Masaburi aliwataka wanachama wa umoja huo kuvunja makundi kwani muda wa majungu umeshaisha.
Katika nafasi zingine zilizogombewa ni vijana iliyochukuliwa na Hawa
Chakoma, Wazazi Mkoa ikienda kwa Amina Mlewa, Baraza Kuu la UWT Taifa
ikienda kwa Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Angellah Kairuki, nafasi
ya mkutano mkuu wa CCM Taifa ikienda kwa Dorothy Kilave.
Katika hatua nyingine, vurugu kubwa zimeibuka katika uchaguzi wa
kuwania nafasi ya Baraza Kuu na Mkutano Mkuu Taifa uliofanyika jana
katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam baada ya wapambe wa
wagombea wawili kuchapana makonde hadharani.
Uchaguzi huo uliokuwa ukitafuta wawakilishi wa nafasi mbalimbali za
Umoja wa Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam na kusimamiwa na Mbunge wa Ilala,
Musa Zungu, ulilazimika kurudiwa baada ya wagombea wawili kupata alama
sawa.
Kabla ya kurudi katika ukumbi wa uchaguzi majira ya saa 9:10, vurugu
zilianza kujitokeza ambapo wapambe wa mgombea Salim Salim ‘Chicago’
walikuwa wakihaha kuhakikisha anaibuka kidedea.
Hata hivyo mpambe wa mgombea mwingine, Nicolaus Msemo, alikuwa makini
na kumfuata mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Idd Toatoa na kuanza
kupigana naye kabla ya kuamuliwa na wanachama waliokuwa karibu yao.
Nafasi ya uwakilishi wa Baraza Kuu mkutano mkuu Taifa kupitia Jumuiya
ya Wazazi mkoa huo ilikuwa ikiwaniwa na wagombea wanne ambao ni Salim
Chicago, Msemo, Mohmed Honelo na Tambwe Hizza.
Honelo na Tambwe walienguliwa mapema kutokana na kura zao kuwa chache huku wagombea hao wawili wakirudi katika uchaguzi.
Aidha, nafasi ya uenyekiti Umoja wa Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam
ikichukuliwa na Mbunge wa Afrika Mashariki, Angela Kiziga aliyeibuka
kidedea kwa kura 170.
|
No comments:
Post a Comment