|
MEYA wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, amesema wananchi wanatakiwa kutimiza wajibu wao, ili nchi ipate maendeleo kwa haraka.
Amesema kama kila mmoja atatimiza wajibu wake na kuondokana na tabia
ya kuitegemea serikali ifanye kila kitu, nchi itapata maendeleo haraka
tofauti na inavyotarajiwa.
Silaa alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akifunga
maonesho ya kifedha na uwekezaji yaliyokuwa yakizishirikisha taasisi
mbalimbali zinazotoa huduma za kifedha.
“Maonesho haya yamefanyika kwa mara ya kwanza nchini, lakini naamini
washiriki wote wamefika hapa kama sehemu ya kila mmoja kutimiza wajibu
wake.
“Kila mmoja akitimiza wajibu wake naamini nchi itasonga mbele, kwa
hiyo, tuondokane na tabia ya kuitegemea serikali katika kila jambo kwa
sababu serikali ina mambo mengi,” alisema Silaa.
Naye Meneja Matukio wa Kampuni ya Neubrand iliyoandaa maonesho hayo,
Geofrey Kivamba, alisema waliamua kuandaa maonesho hayo, ili wananchi
waweze kujua namna huduma za kifedha zinavyotolewa na kampuni
mbalimbali.
Wakati huohuo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imetahadharisha wananchi kuhusu uwepo wa simu feki madukani.
Tahadhari hiyo ilitolewa na Kaimu Meneja Mawasiliano wa TCRA, Semu
Mwakyanjala, katika maonesho hayo na kuwataka wananchi kuwa makini pindi
wanaponunua simu.
|
No comments:
Post a Comment