|
HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali
pingamizi lilowasilishwa mbele yake na Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, lililokuwa
likiomba mahakama hiyo ifute kesi ya madai iliyofunguliwa na Rose Kamili
Slaa aliyeomba imzuie mumewe Dk. Slaa asifunge ndoa na mchumba wake,
Josephine Mushumbusi.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Laurence Kaduri ambaye alisema
baada ya kupitia kwa kina pingamizi lilowasilishwa na Dk. Slaa na majibu
yaliyojibiwa na mlalamikaji Rose anayetetewa na wakili wa kujitegemea
Joseph Thadayo, ameona hoja za kutaka mahakama iifute kesi ya msingi
iliyofunguliwa na Rose ni dhahifu na hivyo amezitupilia mbali.
Jaji Kaduli alisema Dk. Slaa alikosea kudai kuwa Rose hakuwa na haki
ya kufungua kesi hiyo ya kumzuia asifunge ndoa na mchumba wake,
Josephine, kwa sababu hawakuwahi kufunga ndoa ila kulikuwa na dhana ya
ndoa.
“Mahakama hii inaitupilia mbali tena kwa gharama pingamizi hilo la Dk.
Slaa linalosema kuwa Rose hakuwa na haki ya kupinga ndoa yake kwa
sababu hakuwa mke wake na wala hawajawahi kufunga ndoa kwa sababu sheria
ya ndoa inasema mtu ambaye umeishawahi kuishi kama mke na mume kwa
zaidi ya miaka miwili, inawahesabu kama ni wana ndoa.
“Hivyo mahakama hii inasema Rose ana haki ya kufungua kesi ya kuzuia
ndoa ya wadaiwa, yaani Slaa na Josephine na natupilia mbali pingamizi la
Slaa na kwamba kesi ya msingi itakuja kutajwa mahakamani hapa Novemba 6
mwaka huu,” alisema Jaji Kaduri.
Kesi hiyo ya madai ya ndoa ilifunguliwa mahakamani hapo na Rose dhidi
ya Dk. Slaa na Josephine kwa mara ya kwanza mapema Julai mwaka huu,
akiiomba mahakama isikubali shauri hilo lipelekwe kwenye Bodi ya
Maridhiano ya Masuala ya Ndoa kwa ajili ya kupatanishwa.
Dai la pili, Rose anaiomba mahakama itangaze yeye na Dk. Slaa bado ni
wanandoa, na dai la tatu anaiomba mahakama itamke kuwa ndoa baina yake
na Dk. Slaa bado halali kisheria na kwamba ndoa nyingine itakayofungwa
kinyume na sasa itakuwa ni batili. Katika dai lake la nne, mlalamikaji
ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), anadai mdaiwa wa pili
(Josephine) alimshawishi mumewe kuivuruga ndoa yake.
Pia nia ya wadaiwa hao wawili ya kutaka kufunga ndoa waliyopanga
ifungwe Julai 21 mwaka huu katika eneo lolote lile, ndoa hiyo ihesabike
kuwa ni batili.
Aidha, anaiomba mahakama iwaamuru wadaiwa wamlipe fidia ya shilingi
milioni 50 kama gharama za matunzo ya watoto wawili ambao ni Emiliana
Slaa na Linus Slaa aliyezaliwa mwaka 1987 ambao amekuwa akiwahudumia
tangu mwaka 2009 baada ya mume wake kumkimbia.
Pia anaiomba mahakama imwamuru mdaiwa wa pili (Josephine) amlipe fidia
ya sh mil. 500 kwa sababu alimsababishia usumbufu mkubwa na kumharibia
ndoa yake, na kuongeza kwa kuiomba mahakama hiyo impatie nafuu nyingine
ambazo itaona inafaa.
|
No comments:
Post a Comment