|
MOJA ya kosa kubwa watakalolirudia viongozi wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu
wa 2015, ni
kukubali mtego wa kuwapokea na kuwapatia uongozi wafuasi wa CCM waliobwagwa kwenye uchaguzi wa ndani unaoendelea.
Nasema hilo ni kosa kubwa na natabiri mapema kuwa yatakayowafika
watajuta akini wakati huo haitakuwa na faida tena kwao maana watakuwa
wamepigwa mweleka tayari.
Ni kweli kila mtu ana haki ya kujiunga na chama chochote wakati wowote
anaoona unafaa lakini kwa wanachama hawa wa CCM wanaongojea kwanza
kukosa ushindi ndani ya chama chao ndipo watafute hifadhi CHADEMA,
hawafai.
CHADEMA wanatambua ninachokisema kuwa kwenye uchaguzi mkuu wa 2010
katika maeneo mengi walifanya makosa makubwa kama hayo kwa kuwapokea
wana-CCM waliojeruhiwa kwenye uchaguzi wa ndani kisha wao wakawapokea na
kuwapa nafasi ya kugombea udiwani na ubunge na matokeo yake wameyaona.
Leo wako baadhi ya watu hao ndani ya CHADEMA wameshinda ubunge na
udiwani lakini matendo yao ni ya kutaka kukiyumbisha chama kwani hawana
cha kupoteza. Wanajua mkakati wao ukifanikiwa CHADEMA ikapasuka
watapongezwa na CCM kwa kupewa vyeo hata serikalini.
Uchaguzi ndani ya CCM unaendelea na tayari vigogo wenye majina makubwa
wameangukia pua, sasa wanahaha kurejesha heshima zao kwenye taswira ya
kisiasa. Hawa eti wanataka kuhamia CHADEMA. Hivi kweli wana nia ya
dhati?
Kwangu nasema hapana. Hawa si wanasiasa wenye mapenzi mema na Taifa
wala CHADEMA,bali kiu yao ni madaraka. Hivyo iko siku hata ndani ya
CHADEMA wakishindwa watakimbia tena.
Kwangu mimi mwanasiasa makini na mkomavu ni yule anayekubali kuwa wako
watu wengine ndani ya chama chake wanafaa kuongoza kama yeye. Hivyo
hata
akishindwa kwenye uchaguzi hatakimbia ila atazidi kujipanga kwa
uchaguzi mwingine.
CHADEMA kwa sasa ndilo tumaini pekee la Watanzania wapenda mageuzi.
Hiki ndicho chama pekee mbadala kimeweza kuikabili CCM na hivyo
kinastahili kupewa dola lakini kamwe kisikubali kutegwa kupokea majeruhi
wa CCM na kudanganyika kuwapa uongozi.
Anayeipenda CHADEMA na kutaka kuleta mageuzi hapaswi kungoja mpaka
chama chake kimfukuze au ashindwe uchaguzi, isipokuwa anapaswa kuamua
mapema kwa hiari yake na kjiunga na makamanda wapambanaji.
Hawa wanaotaka kukimbilia leo kwa sababu tu wamenyimwa uongozi CCM ni
wabinafsi, wasio na uvumulivu, wepesi wa kuhadaika. Kama CHADEMA itainia
mkenge wao ikawaona wa maana na kuwachukua basi tujipe muda mfupi nayo
itakuwa imegawanyika mapande kama CCM.
Kama wafuasi hawa wanahama CCM kwa vile makundi yao ya kusaka urais
2015 hayajashinda, ina maana hata ndani ya CHADEMA watakwenda
kutengeneza makundi hayo hayo.
Chonde chonde tuachane nao na hata wakiingia tuwaone kama wanachama na kawaida.
Wako wana-CHADEMA wamepifia chama tangu kinaanzishwa hadi leo
hawajapata madaraka makubwa, sasa kwanini wakimbilie kuwachukua
walioshindikana CCM na kuwapachika madaraka pasipo kujihoji endapo
wametumwa kukisambaratisha chama?
Kwa mwaka 2005 CHADEMA tunaweza kuwatetea kuwa walilazimika kuokoteza
kila mtu hata wakawapokea wale waliotemwa CCM na kuwasimamisha wagombee
lakini majibu waliyapata mapema kwani wako waliopewa fedha wakajitoa na
kurejea CCM
na wengine wakafanya kila aina ya hadaa na mwishowe CHADEMA ikala
mweleka.
Tangu mwaka huo hadi leo, CHADEMA imefanya oparesheni za kila aina
mijini na vijijini, imejiongezea mtaji wa wafuasi wenye sifa za kuwania
nafasi zozote
zitakazotakiwa, hivyo hawa ndiyo wanapaswa kupewa kipaumbele badala ya
kukimbilia kupokea wale wenye sura mbili.
Kama itabidi kuwapokea wafuasi hao walioangushwa ndani ya CCM, dawa ya
CHADEMA inapaswa kuwa laini kwamba wabakie wanachama wa kawaidi ila
wakirogwa kuwapa vyeo wakafika juu na kuzisoma siri zao hakika kutakuwa
na kilio cha kusaga meno.
Mifano iko mingi sana ya watu wa aina hii ambao mwaka 2005 walinyimwa
uteuzi CCM wakakimbilia CHADEMA na kupewa nafasi kugombea ila
waliposhindwa wakarejea tena CCM. Sasa hawa tunawaitaje kama si 'wasaka
madaraka'?
Wanasiasa wetu wanapaswa kujifunza jambo moja kubwa kwamba nje ya
madaraka kuna maisha. Hivyo kushinda ama kushindwa katika uchaguzi ni
jambo la kawaida lisilowalazimu kuhama vyama kwa vile hawakuchaguliwa.
Orodha ya wana-CCM walihama kwenda upinzani ni ndefu sana tangu
kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, lakini watu hawa ebu tujiulize
wengi wao wako
wapi? Si hawa walipewa fedha na kuahidiwa madaraka ndani ya CCM na
serikalini wakakimbia upinzani. Sasa hawa wanaotaka kuja CHADEMA baada
ya kushindwa uchaguzi wanatofauti gani na hao wengine? Tafakari!
|
No comments:
Post a Comment