|
RAIS Jakaya Kikwete, amesema kuwa licha ya tukio la kijana wa
Kikristo kukojolea kitabu kitakatifu cha Kuran kuudhi, lakini vurugu za
kulipiza kisasi kwa kuchoma makanisa zinapaswa kuepukwa kwa vile si
suluhu ya tatizo.
Akihutubia katika kilele cha kuzima Mwenge wa Uhuru, sherehe
zilizokwenda sambamba na kumbukumbu za maadhimisho ya miaka 13 ya kifo
cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, mjini Shinyanga, Rais
Kikwete alisema amechukizwa na hatua za watu kujichukulia sheria
mkononi.
Kauli ya rais inakuja ikiwa ni siku tatu tangu vurugu kubwa kutokea
eneo la Mbagala Kizuiani jijini Dar es Salaam na kusababisha makanisa
saba na magari kadhaa kuharibiwa, baada ya mtoto Emmanuel Josephat (14)
kudaiwa kukojolea kitabu hicho kitakatifu kinachotumiwa na Waislamu.
Rais Kikwete aliwaeleza wananchi kuwa ametembelea eneo hilo na
kusisitiza kuwa kitendo hicho cha viongozi wa dini kuwahamasisha wafuasi
wao kujichukulia sheria mkononi hakikuwa sahihi, kwa sababu kijana huyo
alifanya tendo hilo bila kushurutishwa na kundi wala mtu yeyote.
Aliongeza kuwa iko haja ya wafuasi hao kujizuia na kutuliza hasira zao
kwa kutafakari kwanza kwani hata kijana mwenyewe tayari alikuwa
mikononi mwa Jeshi la Polisi.
“Kitendo cha kundi hilo la waumini wa Kiislamu kuingilia kazi za
vyombo vya dola hakikuwa sahihi, kwa sababu kimesababisha mambo ya
kusikitisha na yasiyokuwa na maelezo ya kujitosheleza ndani ya jamii.
“Niliwasihi kuwa pamoja na hasira walizokuwa nazo wawe na subira na
kuvumiliana wakati viongozi wa dini zote mbili wanapojiandaa kukutana na
kufikia muafaka,” aliongeza.
Rais Kikwete aliwataka wananchi wajiepushe na vitendo vya kuchochea
vurugu na uvunjifu wa amani katika nchi, hivyo akawashauri wasichukue
uamuzi wa hasira wakati wa tatizo kwa sababu kwa vyovyote vile ni lazima
watadondokea kwenye makosa.
Alisema vijana 122 wanaodaiwa kutoka kundi la harakati za Kiislamu
wakiwemo 36 vinara wakuu wa vurugu hizo, wanashikiliwa na polisi.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete aliwahamasisha Watanzania
kuendelea kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kwenye tume inayoratibu
maoni bila kushawishiwa kwa ulaghai wa aina yoyote, kwamba hiyo ni haki
na utashi wa kila mtu.
Akemea rushwa
Rais Kikwete katika hilo, aliwataka wananchi wote kuchukua jukumu la
kupambana na vitendo vya rushwa pasipo kuwaachia kazi hiyo Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Alisema vita hiyo ni ya kila mtu huku akiwapiga vijembe wale
wanaolalamika uwepo wa vitendo hivyo pasipo kuchukuwa jukumu la kuwataja
hadharani wahusika ili wachukuliwe hatua.
“Kama tunaendelea kulalamikia rushwa bila kuwataja wala rushwa haiwezi
kutusaidia kuitokomeza. Rushwa ni hatari hasa inapoingia hata kwenye
vyombo vya kusimamia sheria na kutoa haki,” alisema.
CCM watoa kauli
Wakati huo huo, Chama Cha Mapinduzi, kupitia kwa Katibu wa
Halmashauri Kuu (NEC) Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kimelaani
vurugu za kidini zilizotokea Mbagala Kizuiani.
Alisema kuwa CCM kinalaani tukio la kukojelewa kwa kitabu kitakatifu
cha Kuran na vile vile vitendo vya kuvamiwa na kuchomwa moto makanisa na
uporaji wa mali, akisisitiza kuwa havifanani na mila na desturi za
Watanzania.
“Kitendo cha kukojolea kitabu kitakatifu cha Waislamu hakikubaliki, na
kitendo cha kuvamia na kuchoma moto nyumba za ibada za Wakristo na
kufanya vurugu pia hakikubaliki,” alisema
|
No comments:
Post a Comment