|
MTOTO wa Baba wa Taifa, Makongoro Nyerere, ameangushwa katika
kinyang’anyiro cha kutetea nafasi yake ya Mwenyekiti wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, ambayo sasa imechukuliwa na Christopher
Sanya.
Makongoro ambaye amekuwa mwenyekiti wa mkoa huo kwa miaka mitano,
alishindwa katika uchaguzi huo uliofanyika juzi chini ya usimamizi wa
Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) Taifa kutoka Mkoa wa Kagera, Nasir
Karamagi.
Akitangaza matokeo ya awali, Karamagi alisema kuwa kati ya kura 1,012
zilizopigwa, Sanya alipata 469 na Makongoro alijikusanyia 402 huku Enock
Chambili akiambulia 144.
Lakini kwa mujibu wa Katiba ya CCM mshindi hakuwa amevuka nusu ya
kura, na hivyo ilibidi Sanya na Makongoro, kuingia katika duru ya pili
ambapo mwenyekiti huyo anayemaliza muda wake alipitwa kwa kura 59.
Akizungumza baada ya matokeo kutangazwa, Makongoro alimuasa Sanya
kufanya kazi kwa mujibu wa katiba ya chama na kuvunja makundi
yaliyoshamiri ndani ya CCM huku akiahidi kutoa ushirikiano wake.
“Naomba uwe muadilifu, mkoa huu wa Mara ni mgumu sana kuufanyia kazi,
kwani kazi ya uenyekiti si lelemama, hii ndiyo nafasi kubwa ambayo
itatusaidia katika uchaguzi wa 2014/2015,” alisema.
Makongoro aliwataka pia wajumbe kuachana na mambo ya kambi, akisema
uchaguzi umekwisha kilichopo ni kushikamana na kuwapa ushirikiano
viongozi wapya wakiongoze chama vizuri.
Katika nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM mkoa - kila wilaya
nafasi mbili, waliopenya ni Josephat Seronga na Ester Nyarobi
(Serengeti), Zuhura Makongoro na Jackson Waryoba (Bunda), Josehat Kisusi
na Felister Nyambaya (Rorya).
Wengine ni Grace Bunyinyiga na Thabita Idd (Butiama), Abdalah Jumapili
na Kananda Kananda (Musoma Mjini) na Mariam Mkono na Samson Gesase
(Tarime).
Kamani ang’ara Simiyu
Mbunge wa Busega, Dk. Titus Kamani, amepata ushindi wa kishindo
katika kinyanganyiro cha uenyekiti Mkoa mpya wa Simiyu baada ya
kujizolea kura 415.
Waliobwagwa ni aliyekuwa Mbunge wa Afrika Mashariki, George Nangale na Mwenyekiti mstaafu wa CCM Wilaya ya Meatu, Enock Yacob.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Jackson Msome, alisema kuwa kati ya kura
714 zilizopigwa, mbali na Dk. Kamani, Nangale alipata 234 huku Enock
akiambulia 91.
Wakasuvi arejea Tabora
Mwenyekiti CCM Mkoa wa Tabora aliyemaliza muda wake, Hassan Wakasuvi, amefanikiwa kutetea kiti hicho kwa ushindi wa kishindo.
Wakasuvi aliwamwaga wenzake watatu ambao ni Zuberi Mwamba, Juma Nkumba
na Haji Bagio ambao walijitoa muda mfupi kabla ya uchaguzi kuanza.
Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo, Mwigulu Mchemba,
alisema kati ya kura 996 zilizopigwa, Wakasuvi alipata 921, akifuatiwa
na Zuberi Mwamba kura 75 na 16 ziliharibika.
Katika nasaha zake, Wakasuvi aliwataka wajumbe wavunje makundi na
wamsaidie kukijenga chama, huku akiahidi kushirikiana na kila mmoja bila
kujali makovu ya uchaguzi.
Alionya kuwa wapo watu ambao wanadhani kwamba bila wao CCM Tabora
haipo, akisema atawachukulia hatua maana ndani ya chama wamekuwa
wakiketi vikao vya kukibomoa.
Msukuma apeta Geita
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Joseph
Msukuma, aliyeng’olewa madarakani na Baraza la Madiwani kwa tuhuma za
ufisadi, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa CCM Mkoa mpya wa
Geita.
Katika uchaguzi huo, Msukuma alipata kura 565 kati ya 698 zilizopigwa
na wajumbe wa wilaya tano za Nyang'hwale, Geita, Chato, Mbogwe na
Bukombe zinazounda mkoa huo.
Msukuma aliwabwaga Jeremiah Ikangala, aliyepata kura 130 na Mwenyekiti
wa CCM Wilaya hiyo aliyemaliza muda wake, John Luhemeja aliyeambulia
kura tano.
Mlao arudi Pwani
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, aliyemaliza muda wake, Mwinshehe
Mlao, amefanikiwa kutetea kiti chake baada ya kuibuka na ushindi wa kura
528 dhidi ya Kapteni Mpembenue Seif Ally aliyepata kura 196 na Mziwanda
Yahaya aliyeambulia 13.
Washindi wa ujumbe wa NEC kutoka wilayani ni Halfan Mavala, Asia
Madima (Kibaha Vijijini), Fatma Ngozi, Mwajuma Denge (Bagamoyo), Hafsa
Kilingo, Imani Madega (Kibaha Mjini) na Bakari Mbonde, Hawa Mtopa
(Rufiji).
Kingunge anena
Kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru, amesema kuwa vitendo
vya rushwa ndani ya chama hicho, vimeshamiri kutokana na ubinafsi wa
baadhi ya wanachama kuweka mbele maslahi binafsi.
Mzee Kingunge, alitoa kauli hiyo juzi mkoani Pwani, wakati akifungua
mkutano wa uchaguzi wa mkoa wa chama hicho, akisema kuwa ubinafsi huo
umefanya vyama kuwa mali ya mtu na ushindani unakuwa si wa kindugu bali
uhasama.
Alisema wakati wa Afro- Shiraz na TANU, nchi iliwekwa mbele tofauti na
sasa ambapo ubinafsi ndio unawekwa mbele na nchi inabaki peke yake.
“Kwa kuwa suala ni ubinafsi ndiyo maana sasa watu wanafikia hatua ya
kununua vyeo kutoka kwa wapiga kura, jambo linalomdhalilisha mtoaji na
mpokeaji wa rushwa,”alisema.
JK ashauriwa
Mmoja wa wagombea wa Ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) Taifa ya CCM
kupitia Wilaya ya Bunda, Cyprian Musiba, amemshauri Mwenyekiti wa chama,
Rais Jakaya Kikwete, kuwafutia matokeo baadhi ya wagombea waliopita kwa
rushwa.
Musiba ambaye ni mwanahabari kitaaluma na Mkurugenzi wa kampuni ya
mawasiliano ya I&RH, alitaja nafasi ambazo Rais Kikwete anapaswa
kutengua matokeo yake kuwa ni ya Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara na Morogoro.
Pia Musiba alitaja washindi wa nafasi ya ujumbe wa NEC katika wilaya
za Monduli, Bunda na Musoma Mjini pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa
Mara.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Musiba
alifafanua kuwa wenye fedha wameifanya CCM kuwa sehemu ya kufichia
madhambi yao, hivyo hawaoni hatari kutumia gharama yoyote kupata
uongozi.
“Penye rushwa hakuna haki, hakuna kuwatumikia wananchi, mimi ni
miongoni mwa wagombea nilioshuhudia hali hii, watu kutoa fedha kwa ajili
ya kununua uongozi ni jambo la kawaida kwa CCM. Mkoani mara zimetumika
zaidi ya milioni 300 kwa ajili ya kumwangusha Makongoro,” alisema
Musiba.
Kada huyo ambaye wiki iliyopita aliwasilisha malalamiko yake ndani ya
chama kupinga uchaguzi aliyoshiriki wilayani Bunda, alishauri kuwa rufaa
hizo hazipaswi kusikilizwa na kamati za siasa na maadili za wilaya kwa
vile wajumbe wake ndio watuhumiwa.
Alisisitiza kuwa katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara, fedha
zilikuwa zikigawiwa wazi wazi kwa wajumbe na baadhi ya vigogo na
wafanyabiashara wakubwa kuhakikisha watu wao wanashinda.
“Viongozi wanaotumia fedha ndani ya CCM hawawezi kuwa watetezi wa
wanyonge. Na kwa rushwa hii hata uchaguzi wa Bunda kanuni zilikiukwa kwa
kuruhusu mfanyakazi wa serikali kugombea,” alisema.
Musiba alisema kuwa anaungana na kauli ya Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ya kutaka wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi
ndani ya CCM wawajibishwe kwa kutoswa.
Alisema ni fursa nzuri kwa NEC mpya aliyosema ina sura nyingi ngeni
kutomuonea mtu aibu kwa lengo la kukinusuru chama kutokana na kutekwa na
mafisadi hali aliyosema inazidi kukiangamiza.
|
No comments:
Post a Comment