|
JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) jana lililazimika kuingia
mtaani katika jitihada za kuzima ghasia kubwa zilizoligeuza eneo zima la
Kariakoo jijini Dar es Salaam kuwa uwanja wa mapambano.
Mapambano yalizuka baada ya kundi la wafuasi wa kiongozi wa Jumuia na
Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, waliotaka kuandamana
kuelekea Ikulu jijini Dar es Salaam kupinga kukamatwa kwa viongozi wao.
Askari wa JWTZ waliokuwa katika magari matano, wakiwa wamesheheni zana
za kivita, waliwasili katika eneo la Kariakoo, na wengine kuelekea
Ikulu kudhibiti maandamano ya wafuasi hao.
Rais Jakaya Kikwete aliyewasili Ikulu majira ya saa 7:48 mchana
alilakiwa na ulinzi mkali wa askari wa JWTZ, huku mmoja wa wafuasi hao
akiwa anashikiliwa na polisi.
Wafuasi hao pia walikuwa na chupa za maji, miswaki na sabuni ndani ya kanzu zao wakionekana kuwa tayari kwa lolote.
Vurugu hizo zilianza majira ya saa 7 mchana katika Mtaa wa Msimbazi
jirani na Kituo cha Polisi, mara baada ya Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa
katika Msikiti wa Idrisa, ambapo waumini hao waligawiwa vipeperushi vya
kuwahimiza kuandamana kuelekea Ikulu.
Wafuasi hao walizidi kuongezeka baada ya kuungana na wenzao waliotoka
katika Msikiti wa Kwamtoro na hivyo kufanya mapambano kuwa makali zaidi,
huku baadhi ya watu wanaoaminika kuwa wezi na vibaka wakipora bidhaa
mbalimbali za wafanyabiashara.
Ghasia hizo zilisababisha kusimama kwa shughuli zote za kijamii, na kulazimika kufungwa kwa barabara zote katika eneo hilo.
Wakati hali ikizidi kuwa tete, ndipo magari matano yaliyokuwa yamebeba
askari wa JWTZ wakiwa na silaha za moto yaliwasili katika eneo hilo kwa
mbwembwe.
Askari hao walionekana kuwa tayari kwa lolote, lakini hawakuweza
kuanza mapambano yoyote wala kutumia silaha kukabiliana na wafuasi hao.
Katika vurugu hizo zaidi ya watu 100 wamekamatwa.
Waandamanaji hao walikuwa wamebeba vipeperushi vilivyokuwa na
maandishi ya kupinga kukamatwa kwa Waislamu na kuteswa, akina mama
kudhalilishwa na kuwekwa ndani, misikiti kupigwa mabomu Mbagala, Polisi
kuingia na viatu msikitini na kulaani hatua ya Rais Kikwete kuwapa pole
Wakristo katika sakata la vurugu za Mbagala.
Mmoja wa wafuasi waliokamatwa katika eneo la Ikulu aliwaeleza askari
waliomkamata kuwa alikuwa tayari kufa na kwenda peponi kwa madai kuwa
alikuwa akishiriki vita ya jihadi kwa ajili ya Allah.
Zanzibar hakukaliki
Huko Zanzibar, hali ya usalama iliendelea kutoweka kufuatia
kuongezeka kwa ghasia zinazoaminika kufanywa na wafuasi wa kundi la
Uamsho.
Wafuasi wa kundi hilo juzi usiku walivamia makaburi ya Wakristo na
kuyaharibu ikiwa ni pamoja na kubomoa misalaba, huku wakitishia kuchoma
moto Kanisa la Anglikana.
Watu hao pia waliharibu hosteli inayomilikiwa na Kanisa la Anglikana Mkunazini, huku wakitishia kufanya uharibifu zaidi.
Kutokana na hali kuwa tete zaidi, baadhi ya wakazi wa Unguja ambao ni
Wakristo wameanza kuukimbia mji huo, ambapo jana zaidi ya watu 60
waliwasili katika bandari ya Dar es Salaam.
Kuchafuka kwa hali hiyo kumeiweka Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika
wakati mgumu hasa kufuatia hatua ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
kutoka CCM kususia vikao vyake juzi wakipinga ghasia hizo na kuwataka
wakuu wa Jeshi la Polisi Tanzania Bara na Zanzibar kujiuzulu.
Mihadhara yapigwa marufuku
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mecky Sadiki,
amepiga marufuku mihadhara yote ya dini mpaka hali ya usalama
itakaporejea.
Alizungumza hayo jana katika mkutano uliowajumuisha Kamanda wa Polisi
Kanda Maalum, Suleiman Kova, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa
Salum na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu (TEC), Padri Anthony Makunde
na kuzitaka mamlaka zote zinazoshughulika na utoaji vibali vya
mihadhara hiyo kuacha kufanya hivyo.
Naye Padre Makunde alitoa rai kwa Watanzania kuendelea kuvumilia na
kudumisha upendo na mshikamano uliopo miaka mingi baina yao na kusema
kuwa njia pekee ya kufikia suluhu ni mazungumzo bila jazba na hasira.
Kwa upande wake Sheikh Alhad aliwataka Waislamu, maimamu na masheikh
kuwa na subira na kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani na
kutojidanganya kuwa na jihad kwani haiji kwa uvunjifu wa sheria na
kwamba nidhamu ya dini hiyo na utaratibu wake unakataa vitendo hivyo.
Lwaitama aishukia serikali
Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Azavel Lwaitama,
amesema udhaifu wa serikali ndio umefanya suala la vurugu za
wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Kiislamu kulifikisha taifa hapa lilipo.
Udhaifu huo Lwaitama alisema ulianza tangu katika kipindi cha fujo za
Mwembechai ambapo serikali haijaonesha jitihada zozote za kulitafutia
suala hilo ufumbuzi.
Kutokana na hali hiyo, Lwaitama alitaka busara itumike zaidi katika
kutatua fujo zinazoendelea sasa hivi badala ya kutumia nguvu kwani
inaweza kuifikisha nchi pahali pasipotarajiwa.
Alisema kitendo cha kukamatwa kwa Sheikh Ponda sasa hivi na kusomewa
mashitaka ya matukio yaliyotendeka tangu huko nyuma baada tu ya kuvamia
kiwanja ni kama kutaka kuficha kitu nyuma ya pazia.
“Mimi naishangaa sana hii serikali kwani wakati matukio yale ya nyuma
yalipotokea walikuwa wanashindwa nini kumkamata Sheikh huyo? Hebu
katika hili busara zaidi itumike kwani na yeye ana wafuasi wake wengi
hivyo watakapoamua kuingia barabarani hakuna atakayesalimika,” alisema.
Pia hakusita kuwapongeza viongozi wa madhehebu ya Kikristu kwa hatua
yao walioichukua ya kuwa wavumilivu katika kipindi hiki na kukazana na
maombi.
Kuhusu mtoto aliyekojolea msaafu, Lwaitama alisema hayo yote
yametokana na matukio ya mfumo wa elimu uliopo sasa hivi hapa nchini wa
kutoheshimu dini za wenzao.
Alisema umri wa mtoto huyo wa miaka 14 sio mdogo kihivyo kiasi cha
kushindwa kutambua kile alichokuwa anakifanya ni kosa na badala yake
alisema elimu wanayopewa watoto siku hizi haiwajengi katika kuweza
kuishi na watu tofauti kwenye jamii.
Kova akanusha
Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi, Suleiman Kova amekanusha taarifa
iliyotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa Jeshi la Polisi
limewataka Waislamu wote wa kikundi hicho kujisalimisha kwa jeshi hilo.
Kova alisema kuwa watu wanaotakiwa kujisalimisha ni sita na kuwataja
kuwa ni Mukadam Saleh Kondo, Saleh Juma Bungo, Shaaban Mapeo, Jaafar
Mneki, Rajab Katimba na Amani Moshi.
Hadi tunakwenda mitamboni, hali katika mitaa mingi ya Kariakoo ilikuwa
haijatulia na kulikuwa na wasiwasi kwamba, watu hao walikuwa
wakijikusanya kuendeleza mapambano na polisi.
|
No comments:
Post a Comment