Saturday, October 20, 2012

Ulimboka amefungua milango ya uchunguzi




VYOMBO vingi vya habari juzi vimetawaliwa na habari inayomhusu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka, ambaye ameweka bayana kile kilichomsibu usiku wa Juni 26 mwaka huu, katika msitu wa Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Dk. Ulimboka ameeleza mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuwataja kwa majina baadhi ya watendaji wa Ikulu ambao anaamini kuwa walihusika kwa namna moja ama nyingine katika tukio la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwake.
Tunampongeza Dk. Ulimboka kwa kuweka bayana kile anachokiamini kuwa ndiyo ukweli wa tukio la kutekwa kwake, kwani tunadhani sasa atakuwa amefungua milango ya sakata hilo kuchunguzwa kwa umakini kukata mzizi wa fitina.
Ni kweli kesi ya tukio hilo imefunguliwa mahakamani ambapo raia mmoja wa Kenya anashtakiwa kufanya tukio hilo, lakini bado haizuii uchunguzi wa kina kuendelea hasa wakati huu ambapo muhusika amejitokeza wazi kutoa ushirikiano wa kuwatambua wale waliomfanyia kitendo hicho.
Tume ya uchunguzi iliyoundwa na Jeshi la Polisi kuchunguza tukio hio, imekuwa ikinyooshewa kidole na baadhi ya wadau wakiwemo madaktari wenyewe kwa madai kuwa haiko huru kwani baadhi ya wajumbe wake ni watuhumiwa.
Hata Dk. Ulimboka katika taarifa yake hiyo ya jana, amesisitiza kuwa yuko tayari kutoa ushirikiano wa kina endapo kitaundwa chombo huru kuchunguza tukio hilo.
Ni vyema serikali ikajitafakari upya ili kuondoa sintofahamu hii vinywani mwa watu kwa kuunda chombo huru ili kuchunguza sakata hilo na hivyo kumfanya Dk. Ulimboka na Watanzania wengine kujiona wana haki ya kuishi kwa amani katika nchi yao.
Dk. Ulimboka ameeleza wazi kuwa anathibitisha kwamba Ramadhani Ighondu alitambulishwa kwao kwa jina la Abeid. Kwamba Binafsi anamfahamu sana bwana huyu kwa sababu alikuwa akitumwa mara kwa mara kuja kukutana naye na wamekutana mara kadhaa kabla ya tukio lile.
Alisema wazi kuwa anakumbuka kuwa Abeid alitambulishwa kwao na kigogo mmoja, akiwa pamoja na wawakilishi wengine wa madaktari kuwa yeye (Ramadhani Ighondu) ndiye atakayehusika katika kuchukua madai na hoja za madaktari katika mgogoro kati ya madaktari na serikali.
Kwamba anathibitisha kwamba mfanyakazi huyu wa Ikulu, ndiye aliyempigia simu na kumuita kwenye kikao ambako muda mfupi baadaye alitekwa. Katika mawasiliano hayo, Abeid alikuwa anatumia simu namba 0713 760473.
Dk. Ulimboka amebainisha kwamba hakuna shaka kwamba anamtambua Abeid kwa sura na namba aliyokuwa anatumia kuwasiliana naye mpaka siku ya kutekwa kwake.
Hivyo, kwa maelezo hayo ya Dk. Ulimboka, hatuhitaji kuibua mijadala ya malumbano ya nani kafanya nini na nani hakuhusika, isipokuwa jambo la msingi hapa ni kuundwa chombo huru kitakachokuja na majibu ya kumaliza utata huu, ndiyo maana tunasema Dk. Ulimboka amefungua milango ya uchunguzi.

No comments:

Post a Comment