Monday, October 15, 2012

Kada CCM amkomalia Sumaye


KADA wa Chama cha Mapinduzi (CCM), David Msuya, amemtaka Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, kuwataja waliotoa rushwa katika uchaguzi wa viongozi wa CCM mwaka huu.
Msuya ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache baada ya Sumaye kueleza sababu zilizochangia ashindwe uchaguzi wa nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, wilaya ya Hanang, kuwa unatokana na vitendo vya rushwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Msuya ambaye pia ni mkurugenzi wa vikundi vya maendeleo ya wanawake (Inuka), alisema badala ya kulalamika, Sumaye anatakiwa awataje wala rushwa na watoa rushwa walioko ndani ya chama hicho, ili wachukue hatua kwa mujibu wa sheria.
“Sisi Watanzania hatupendi rushwa maana ni adui wa haki, hivyo si busara kuongea tu badala ya kuchukua hatua kwa kuwa yeye ni kiongozi mkubwa mwenye sauti serikalini ambaye kama analalamika na sisi tufanyeje? Kwa hiyo anatakiwa kupeleka suala hilo kwenye vikao vya chama,” alisema.
Aidha, Msuya aliitaka serikali ikae na viongozi wote wa dini katika kukemea vitendo vya vurugu vinavyoweza kujitokeza na kuharibu amani ya nchi kutokana na vurugu za kidini zilizoibuka hivi karibuni ambapo makanisa na vitu mbalimbali ama vimechomwa moto au vimeibiwa.

No comments:

Post a Comment