|
WAKATI sakata la kutekwa, kuteswa na kisha kutupwa katika msitu
wa Mwabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar ss Salaam kwa Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Madaktari Nchini, Dk Steven Ulimboka, likiwa limefikia miezi
mitatu, Ikulu imeibuka na kumkana mtumishi wake Ramadhan Ighondu
anayetajwa kuhusika katika unyama huo.
Mwanzoni mwa wiki Dk. Ulimboka alitoa tamko akisema kwamba Ighondu
ndiye aliyehusika na sakata la kumteka na kumtesa vibaya katika jaribio
la kutaka kumuua.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumamosi, Ikulu jana, Katibu Mkuu
Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, alisema kuwa hamfahamu mtumishi huyo
aliyetajwa na Ulimboka.
Alisisitiza kuwa Ikulu haipo kwa ajili ya kuteka na kutesa watu, hivyo
wale wanaodai kuwa mtumishi wa ofisi hiyo anahusika na tukio hilo
wanaongea tu.
“Wala simfahamu…Ikulu haipo kwa ajili ya kutesa watu na hao wanaomtaja
mtumishi huyo kuwa yupo Ikulu hao wanazungumza tu,” alisema.
Wakati Balozi Sefue akitoa kauli hiyo, juzi Mkurugenzi wa Mawasiliano
Ikulu, Salva Rweyemamu, alisisitiza kuwa Ikulu haihusiki na kwamba Rais
Jakaya Kikwete alishalijibu suala hilo.
Katika tamko lake la kiapo lililotolewa kwa waandishi wa habari, Dk.
Ulimboka, kupitia kwa wakili wa kujitegemea, Nyaronyo Kicheere, alisema
anamfahamu mtesaji wake, na kwamba hata akikamatwa leo hii, atakwenda
kufanya utambuzi.
Alisema anashangaa kwamba polisi wameshindwa kumtia mbaroni mtuhumiwa
huyo, licha ya kwamba alishatajwa na gazeti la MwanaHALISI na katika
mtandao wa YouTube.
Alisema: “Nathibitisha kwamba Ramadhan Ighondu alitambulishwa kwetu
kwa jina la Abeid. Binafsi ninamfahamu sana bwana huyu kwa sababu
alikuwa akitumwa mara kwa mara kuja kukutana na mimi na tumekutana mara
kadhaa kabla ya tukio lile.
“Nathibitisha kwamba mfanyakazi huyu wa Ikulu, ndiye aliyenipigia simu
na kuniita kwenye kikao ambacho muda mfupi baadaye nilitekwa. Katika
mawasiliano hayo, Abeid alikuwa anatumia simu namba 0713 760473.”
Dk. Ulimboka aliongeza kuwa, anakumbuka kuwa Abeid alitambulishwa
kwake na kigogo mmoja, akiwa na wawakilishi wengine wa madaktari, kuwa
ndiye angehusika katika kuchukua madai na hoja za madaktari katika
mgogoro kati yao na serikali.
Kauli ya jana ya Balozi Sefue ni ya tatu kutolewa na Ikulu kuhusu Dk. Ulimboka.
Mara ya kwanza, ilitolewa na Rais Jakaya Kikwete alipokutana na baadhi
ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari ambapo alisema, “Dk.
Ulimboka ana nini mpaka Ikulu imteke? Tumteke ili iweje?”
Kikwete alikwenda mbali zaidi na kusema hata Dk. Ulimboka mwenyewe
alipokwenda Ikulu akiwa na viongozi wenzake, alinyamaza kimya tu na
kwamba waliokuwa wakizungumza ni wengine.
Hata hivyo, kwa kuwa Ikulu imesema haihusiki, na Dk. Ulimboka mwenyewe
ametamka kwamba anamjua aliyemtesa, na kwamba anafanya kazi Ikulu, ni
juu ya umma kuamua nani anasema ukweli.
Juni 26, mwaka huu, Dk. Ulimboka alitekwa, akapigwa, akang’olewa kucha
kabla ya kuokotwa msitu wa Mabwepande na kupelekwa katika Taasisi ya
Mifupa ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Moi) kwa matibabu.
Hata hivyo, baadaye alipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi na alirejea nchini Agosti 12, mwaka huu.
|
huo si utu mwanangu
ReplyDelete