|
NAIBU Katibu Mkuu wa CHADEMA na Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Kabwe Zitto, amesema tuhuma za rushwa zinazoelekezwa kwake ni mkakati
wa makusudi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutaka kuaminisha wananchi
kuwa ufisadi upo pia ndani ya upinzani.
Zitto amedai kuwa kwa bahati mbaya pasipo kujua wako baadhi ya wabunge
wa upinzani nao wameingia kwenye mtego huo wa uzushi wa CCM bila
tahadhari kuwa hiyo ni vita ya kisiasa ya kuisambaratisha CHADEMA.
Mbunge huyo alifichua mbinu hizo jana mjini hapa wakati akizungumza
na waandishi wa habari, kuelezea hatua ya tuhuma za rushwa zilizotolewa
kwenye majadiliano ya Wizara ya Nishati na Madini.
“Nalazimika kukutana nanyi kutoa maelezo juu ya tuhuma zenye shinikizo
la kisiasa zinazoelekezwa kwangu binafsi kwamba hata mimi nimeshiriki
katika vitendo vya rushwa, kwa nafasi yangu kama Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC). Taarifa hizo, kama kawaida ya uzushi
mwingine wowote zimesambazwa kimkakati na kwa kasi kubwa kiasi cha
kuukanganya umma,” alisema.
Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
alisema anawajibika kuwatoa hofu wananchi kutokana na hisia potofu kwa
vile ana dhamana kubwa ya uongozi.
“Mkakati huo wa kuniunganisha na baadhi ya wabunge wanaotuhumiwa kwa
kupokea rushwa unatekelezwa na watendaji wa serikali ambao wamekuwa
wakizieneza habari hizo na hususan kutoa taswira kwamba baadhi ya kauli
zangu zinatokana na ushawishi wa rushwa,” alisema.
Alisema kuwa watu mbalimbali wamefikia kuaminishwa habari hizo kiasi
cha wengine kuuliza kwanini hakutajwa katika orodha iliyotolewa na
Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu, alipowataja wabunge
sita wa CCM wanaotuhumiwa kwa rushwa.
Zitto ambaye aliongozana na wabunge 14 wa CHADEMA katika mkutano huo,
alisema kuwa hiki ni kipindi cha pili cha ubunge na akiwa mwenyekiti wa
POAC, ukiwa ni takriban mwaka wa saba sasa, kwamba kamati yake
inasimamia mashirika 259 ya Umma na si TANESCO peke yake.
“Zipo hoja pandikizi za kutaka POAC ivunjwe na hasa zikinilenga mimi
binafsi. Nafahamu kiu ya wasioitakia mema nchi yetu kuiona POAC
ikivunjwa au sura zikibadilishwa, kwa kuwa kamati hii imekuwa mwiba kwa
mikakati yao ya kifisadi,” alisema.
“Mimi Zitto Zuberi Kabwe sina bei, sijawahi kuwa nayo na sitarajii
kuwa nayo huko mbeleni. Daima nimesimamia kidete maadili ya uongozi bora
katika maisha yangu yote ya siasa, na nawaahidi sitarudi nyuma katika
mapambano dhidi ya rushwa katika nchi hii pamoja na mikakati ya aina hii
ya kunidhoofisha na kunivunja moyo,” alisema.
Aliweka bayana kuwa kwa maoni yake POAC isihusishwe na tuhuma hizo kwa
vyovyote vile kwamba yuko tayari ahukumiwe yeye na si kuhusisha wajumbe
wengine ambao hawatajwi mahala popote katika tuhuma hizo mbaya katika
historia ya Bunge.
“Nitakuwa tayari kuinusuru POAC na masilahi ya taifa letu kwa
kujiuzulu uenyekiti iwapo itathibitika pasipo shaka kuwa nimehongwa.
Kamati ya POAC ni muhimu zaidi kuliko mimi,” alisema mbunge huyo.
Zitto alisema anafahamu kwamba kuna wanasiasa hasa wa upinzani ambao
wanautaka sana uenyekiti wa POAC na wanafanya kila njia kutaka
kuidhoofisha, lakini wanashindwa kuelewa kuwa anayepanga wajumbe wa
kamati ni Spika wa Bunge.
“Msishangae pia kuja baadaye kubaini kwamba baadhi ya wanasiasa wenye
midomo mikubwa ya kutuhumu wenzao wao ndio vinara wa kupokea rushwa,”
aliongeza.
Zitto alisema baada ya bodi ya wakurugenzi ya TANESCO chini ya
uenyekiti wa Meja Jenerali mstaafu Robert Mboma, kutangaza kumsimamisha
kazi Mkurugenzi Mkuu, William Mhando, ili kupisha uchunguzi, POAC
ilimuandikia Spika kumuomba aridhie kuwaita Bodi ya TANESCO, Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na pia Mamlaka ya Udhibiti wa
Manunuzi ya Umma (PPRA) kujiridhisha na tuhuma zote zinazotajwa
zifanyiwe uchunguzi wa kina na hatua kuchukuliwa.
“Tulifanya hivyo kwani kulikuwa na tetesi kuwa kusimamishwa kazi kwa
Mhando siku chache kabla ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini
kulikuwa na lengo la kufunika ‘madudu’ makubwa zaidi kwa kulichagiza
Bunge na tukio hilo dogo, mkakati ambao naona umefanikiwa sana,”
alisema.
Zitto alisema kuwa kitendo hicho cha halali na kwa mujibu wa kanuni
kilichofanywa na kamati yake kimetafsiriwa kwa makusudi na baadhi ya
watu kwamba ni ishara ya kuwa yeye ana masilahi binafsi na TANESCO na
hususan Mhando.
“Baada ya tukio hilo, nikiwa hapa Dodoma, mwandishi wa habari wa
gazeti moja alinifuata akiniambia kuwa wamekutana na Waziri Sospeter
Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliachim Maswi, hapa bungeni na wamewaambia
kuwa mimi nimepewa rushwa. Hakutaja nimepewa rushwa na nani, kiasi gani
na wala kwa lengo gani,” alitanabaisha.
Aliongeza kuwa alijaribu kumtafuta kwa simu Waziri Muhongo na Maswi
ili wampe ufafanuzi juu ya yeye na kamati ya POAC kuhusishwa na tuhuma
hizo bila mafanikio, hali ambayo alidai inamwondolea mashaka juu ya
ushiriki wao katika kueneza au kuthibitisha uvumi huo.
“Binafsi sijawahi kuwa na mawasiliano ya aina yoyote na uongozi wa
TANESCO kushawishiwa juu ya hatua ambazo POAC ndio imezichukua za kutaka
kujiridhisha juu ya utaratibu uliotumika,” alisema.
Alibainisha kuwa hakuna wakati wowote, popote ambapo yeye binafsi au
kamati yao imekataa Mhando kuchunguzwa kwa tuhuma zozote kwamba
wanachosisitiza wakati wote ni ufuatwaji wa taratibu, kanuni na sheria,
jambo alilodai atalisimamia, iwe masika au kiangazi.
Zitto alisema ni kwa sababu hiyo, amekutana na Spika Anne Makinda na
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, juzi na kwamba kwa kujiamini
kabisa amewaomba suala la tuhuma za rushwa zinazotajwa dhidi yake
zichunguzwe na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kina.
“Nimekwenda mbali zaidi kukiomba chama changu CHADEMA kifanye pia
uchunguzi na tathmini yake kwa kina kujiridhisha na tuhuma hizo, natumia
fursa hii pia kuomba vyombo vya dola vichunguze tuhuma hizo kwa nafasi
yake ili kuweza kupata ukweli.
Zitto alisisitiza kuwa lazima wafike mahali kama viongozi kwamba
utaratibu unapokiukwa na yeyote yule, au uongo unapotolewa hadharani
waseme bila kuogopa.
Alisema kuwa kwa imani hiyo, hatasalimu amri mbele ya dhamira zao ovu
hata atakapobaki peke yake katika mapambano hayo ya kulinda na kutetea
rasilimali za taifa zinufaishe Watanzania wote.
Alimtaka Waziri Muhongo kuwaeleza ukweli wananchi kuwa ili mgawo wa
umeme usiwepo tena nchini serikali itapaswa kulipa sh bilioni 42 kila
mwezi kwa kampuni binafsi za kufua umeme za IPTL na Symbion, ukweli
ambao alidai utakuja kujulikana wenyewe muda si mrefu.

|
No comments:
Post a Comment