|
TAARIFA kuwa Bunge limeunda kamati ya kuchunguza wabunge wake
wanaotuhumiwa kwa rushwa iliyofichuliwa na wabunge wenzao, zilionekana
kuwa habari njema.
Lakini, baada ya kuangalia jinsi mizengwe inavyoanza kuchukua nafasi
yake na aina ya watu wanaounda kamati hiyo, waweza kusema hiki ni kiini
macho kutokana na sababu zifuatazo:
Kwanza, wengi wa wajumbe wa kamati hii licha ya kutoka chama kimoja
na watuhumiwa, hawana udhu wala historia ya kuridhisha kufanya kazi hii.
Pili, tuhuma zinazowakabili wahusika ni za jinai. Hivyo, jambo bora
lililostahiki kufanyika si kuwachunguza, bali kuwafikisha mbele ya
vyombo husika vya sheria.
Kama hili haliwezekani au linaonekana kuwa hatari kwa waheshimiwa
kuogopa kuumbuliwa mbele ya mahakama, kwanini mahakama isifanye hivyo
kwa njia ya usiri?
Kinachofanyika ni ubaguzi wa wazi wazi wakati wa kushughulika na watu wanaotuhumiwa kwa makosa ya jinai.
Kanuni ya adhabu iko wazi kuwa kila mtu anayetenda kosa la jinai, lazima afikishwe mahakamani na si kwenye kamati.
Kama watawala wetu wameamua kuvunja sheria na kubagua wananchi ili
kuwalinda wenzao, kwanini isiundwe tume inayohusisha watu wenye udhu
kama vile majaji au Watanzania wanaoaminika na kujulikana kwa udhu na
uzalendo wao badala ya hii danganya toto?
Hakuna haja ya kufikiria juu ya heshima ya wabunge ingawa wakishajihusisha na rushwa heshima yao inapotea.
Kama siyo Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kutekwa na
ofisi ya rais hadi ikapoteza maana kwa kuwa chombo cha kulinda na
kusafisha mafisadi, ingeweza kufanya kazi ya kuwachunguza hata
kuwashitaki watuhumiwa kama wangepatikana na mashtaka.
Lakini, kwa vile TAKUKURU haina heshima wala udhu tena, ingeundwa tume yenye kuwa huru na kuwachunguza hawa watuhumiwa.
Hebu fikiria. Watu wanatuhumiwa kwa rushwa na wanaendelea kukaa
bungeni wakati walipaswa kuwajibishwa kungoja taarifa za uchunguzi. Hii
pekee inatosha kuonesha kuwa haki haitatendeka.
Wabunge wanapotuhumiwa kula rushwa, kwa maana nyingine ni kwamba Bunge limetuhumiwa chini ya dhana ya uwajibikaji wa pamoja.
Hivyo, kuruhusu Bunge kuchunguza wabunge wake wanaotuhumiwa kula
rushwa, ni sawa na kulifanya kuwa mtuhumiwa, mwendesha mashitaka, polisi
mkamataji na hakimu katika kesi inayolikabili.
Hapa, haki haitatendeka zaidi ya kuvuruga mfumo mzima wa utawala wa
sheria kama upo. Bunge linachukuliwa kama mtuhumiwa si kwa maana kuwa
wabunge wote ni wala rushwa. Hasha. Linatuhumiwa kutokana na ubovu wa
mfumo na muundo wake. Kama Watanzania na serikali pamoja na taasisi
nyingine kama Bunge wanachukia rushwa, basi waache sheria ichukue mkondo
wake katika kushughulikia wabunge wanaotuhumiwa kula rushwa.
Bila kufanya hivyo, umma utaona ni kama sanaa na viini macho kama
kawaida. Itajenga picha kuwa wanaojidai wanapambana na rushwa ndio wala
rushwa wenyewe.
Ni pigo kwa haki hasa pale watunga sheria wanapokuwa wala rushwa
wenyewe. Hawa hawawezi kutunga sheria za kupambana na rushwa wala
ufisadi kwa vile wananufaika na jinai hizi.
Inakuwaje watendaji wengine wakituhumiwa wanakamatwa na kuwekwa ndani
huku wakipelekwa mahakamani moja kwa moja, lakini si kwa wabunge
wanaopaswa kuwa mfano?
Je, wabunge wa namna hii wanaweza kutunga sheria za kupambana na kile wanachonufaika nacho?
Je, wabunge wa namna hii wakishirikiana na serikali inayotuhumiwa
kupatikana kwa njia ya kuiba pesa ya umma na kutoa rushwa wanaweza
kuivusha nchi yetu?
Rejea madai ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa, kuwa Rais
Jakaya Kikwete aliingia madarakani kwa kutumia pesa ya wizi toka Akaunti
ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu. Bahati mbaya, pamoja na
kuchagizwa akanushe hata kutoa maelezo kuhusiana na tuhuma hizi, Kikwete
siku zote amegwaya kufanya hivyo kwa kuchelea anaweza kuumbuliwa zaidi.
Tatu, kinachofanyika licha ya kuwa kiini macho na juhudi za kulindana,
ni sawa na kupeleka kesi ya wizi wa mahindi inayomkabili ngedere kwa
ngedere mwenzie au nyani. Hukumu yake inajulikana kuwa ngedere
watashinda tu. Kwa vile mchezo wa mahakimu wao ni ule ule.
Kama upogo huu hautarekebishwa, kuna uwezekano wa wabunge wasiokula
rushwa nao kuanza rushwa. Maana wanajua wakifichuliwa kesi yao
itahukumiwa na wenzao tena wenye kukubuhu kwenye jinai hii.
Nne, wengi wa wajumbe ni wakereketwa na makada wa chama tawala ambacho kinajulikana kwa tabia yake ya kulindana.
Rejea maneno ya Mbunge Anne Kilango aliyekaririwa akisema kuwa wabunge
wanapaswa kulinda maslahi ya chama badala ya maslahi ya nchi.
Alikaririwa akisema: “Tulimtosa Lowassa, baadaye ukweli umejulikana,
na sasa makosa yetu yanaigharimu serikali na CCM. Tusirudie makosa yale
yale, tuwaache hawa kwa maslahi ya CCM.”
Maneno haya ya kifisadi ya Kilango yanaonesha CCM ilivyodhamiria kulinda maslahi yake hata kwa kuhujumu taifa.
Hii ikichangiwa na baadhi ya wanakamati kupata ubunge wao baada ya
kushindwa, lazima watalipa fadhila kwa chama kilichowawezesha.
Nani mara hii kasahau jinsi mjumbe mmojawapo, Gosbert Blandes
alivyotuhumiwa kupewa ushindi wa ubunge mezani kutokana na mchezo mchafu
wa kuchakachua matokeo?
Blandes pia alituhumiwa kutoa hongo kwenye uchaguzi ukiachia mbali
kutokuwa na udhu wa kutosha zaidi ya kupaswa kuchunguzwa yeye mwenyewe.
Wajumbe kama Brigedia mstaafu Hassan Ngwilizi hawawezi kutenda haki
ikizingatiwa kuwa ni wakereketwa wa CCM.
Wajumbe kama John Chiligati wanajulikana walivyo na mamlaka chamani
ukiachia mbali mjumbe kama Riziki Omar Juma kutoka kwenye chama chenye
ushirikiano na CCM.
Tumalizie kwa kuwasihi Watanzania wakatae huu usanii na ushirika
katika ufisadi unaofanywa na taasisi zinazojiita zao wakati si zao, bali
za kikundi kidogo cha watu kilichojihalalishia ulaji kwa gharama zao.
Kundi lililowageuza wanachi punda wa kubeba mizigo yake.
Swali kuu la kujiuliza hapa ni je, Spika wa Bunge, Anna Makinda, Bunge
na wabunge wanataka kumdanganya nani kuwa wanaweza kutuhumiwa,
wakajichunguza au kuchunguzana na kuhukumiani kwa haki?
|
No comments:
Post a Comment