Saturday, August 11, 2012

Mizinga ya JWTZ yazua hofu Dar

WAKAZI wa Kibamba, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, usiku wa kuamkia jana walilazimika kuzikimbia nyumba zao baada ya kutokea kishindo kikubwa cha milipuko katika kambi ya vifaru vya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Mloganzila.
Tukio hilo limetokea majira ya usiku kati ya saa 5 hadi 7:04 ambapo milipuko mitano ya mizinga ilisikika kutoka eneo hilo la Mlongazila katika wilaya jirani ya Kisarawe mkoani Pwani, ikiambatana na kukatika kwa umeme, mawasiliano ya simu na mvua kubwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima, wakazi hao walisema tukio hilo limewashtua kwa sababu halijawahi kutokea katika kipindi cha miaka zaidi ya saba walichoishi kwenye eneo hilo.
Walisema kuwa waliamua kukimbia na kuelekea kusikojulikana kwa lengo la kuokoa maisha yao, kwani walihofia madhara ya milipuko ya mabomu kama ilivyotokea kwenye kambi za Mbagala na Gongo la Mboto.
Mmoja wa wakazi hao, Mhando Yahaya, alisema wakazi wote wa Kibamba walikimbilia kwenye kijiji kidogo cha Kibwegele, wakiacha nyumba pamoja na mali zao bila kujali.
“Ujue serikali inabidi itowe angalizo kabla na si kufanya siri kwa kuwa matokeo yake ni kama haya, wananchi tunatishika na kukimbia hovyo usiku huu, mvua na giza vikituandama,” alisema Yahaya.
Naye Egnes Habiyu, alisema milipuko kama hiyo, imesababisha baadhi ya wagonjwa wa moyo kushtuka hadi kufikia hatua ya kuishiwa nguvu na wengine kujeruhiwa wakati wakikimbia.
Akifafanua kuhusu milipuko hiyo, Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, alisema hayo yalikuwa mazoezi ya kawaida na kwamba hayana uhusiano wowote wa kivita.
Vilevile aliwatoa wasiwasi wananchi kuwa milipuko hiyo haina madhara bali ni moja ya mazoezi ya kawaida.
Kanali Mgawe alisema taarifa zilitolewa mapema kwa wakazi wanaoishi jirani na kambi hiyo, hivyo kwa vile mazoezi yalifanyika usiku kukiwa kumetulia sauti ya milipuko hiyo ilisikika hadi mbali.

Wednesday, August 8, 2012

Kashfa nzito UVCCM Iringa

Kashfa nzito UVCCM Iringa

ZAIDI ya robo tatu ya wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Iringa, wamedaiwa kudanganya umri wao wakati wa ujazaji wa fomu za kuwania nafasi hizo.
Kashfa hiyo imeibuka baada zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu kumalizika juzi.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumatano, umebaini kuwepo kwa udanganyifu wa umri ambao kikomo chake ni miaka (30), huku baadhi ya wagombea wakiwa na umri mkubwa zaidi ya hapo.
Udanganyifu huo wa UVCCM, umesababishwa na ushindani mkubwa uliopo katika jumuiya nyingine za chama hicho mkoani hapa huku nafasi nyeti zote za jumuiya hizo kama ile ya Jumuia ya Wazazi (TAPA) na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), zikienda kwa vigogo.
Mmoja kati ya vijana wanaowania nafasi moja wapo ndani ya UVCCM mkoani hapa ambaye hakupenda kutaja jina lake kwenye vyombo vya habari, alisema UVCCM Iringa imeendelea kupoteza dira yake huku kanuni za umoja huo zikiendelea kufinyangwa na waliopata kuwa viongozi wa umoja huo.
Alisema, viongozi hao bado wanaonekana kung’ang’ania uongozi katika kundi hilo la vijana japo umri wao umevuka hata kwa mwonekano wa kawaida bila uthibitisho wa vyeti vya kuzaliwa.
Mgombea huyo alisema inashangaza kuona vijana wengi wakitumia vyeti vya kuapa mahakamani badala ya vile walivyotumia kipindi cha nyuma ambacho walipata kuomba nafasi za uongozi ndani ya UVCCM na jumuiya nyingine za chama.
“Hivi tunaomba uongozi wa UVCCM mkoa kuwahoji wanachama waliokimbilia kuziba nafasi za vijana wenye sifa ndani ya UVCCM kwa kudanganya miaka yao ya kuzaliwa ...kwani haiwezekani kijana aliyegombea nafasi ya uongozi ndani ya UVCCM mwaka 2007 akiwa na miaka 28 au 27, leo anakuja kugombea tena akiwa na miaka pungufu ya hiyo.
“Ina maana alisimama kukua ili kuja kugombea nafasi hiyo?” alihoji kijana huyo huku akiutupia lawama uongozi wa UVCCM mkoa kukubali kupokea fedha za gharama za fomu kwa wanachama wa UVCCM ambao umri wao umevuka mipaka.
Alisema wapo baadhi ya wagombea waliogombea nafasi za uenyekiti mwaka 2007 wakiwa wamejaza miaka 29, lakini leo wamekuja na umri mdogo zaidi.
Katibu wa UVCCM Iringa, Rhoda George, alisema kila mwanachama wa UVCCM mwenye sifa ya kugombea, anaruhusiwa kuchukua fomu.
Alisema hadi mwanachama kupitishwa kuwa kiongozi, vipo vikao mbalimbali vya uchujaji wa majina ya wagombea ambavyo vinapitia sifa za wote walioomba na iwapo itabainika wamedanganya basi vikao vitaamua.

Makinda anataka kumdanganya nani?

Makinda anataka kumdanganya nani?


TAARIFA kuwa Bunge limeunda kamati ya kuchunguza wabunge wake wanaotuhumiwa kwa rushwa iliyofichuliwa na wabunge wenzao, zilionekana kuwa habari njema.
Lakini, baada ya kuangalia jinsi mizengwe inavyoanza kuchukua nafasi yake na aina ya watu wanaounda kamati hiyo, waweza kusema hiki ni kiini macho kutokana na sababu zifuatazo:
Kwanza, wengi wa wajumbe wa kamati hii licha ya kutoka chama kimoja na watuhumiwa, hawana udhu wala historia ya kuridhisha kufanya kazi hii.
Pili, tuhuma zinazowakabili wahusika ni za jinai. Hivyo, jambo bora lililostahiki kufanyika si kuwachunguza, bali kuwafikisha mbele ya vyombo husika vya sheria.
Kama hili haliwezekani au linaonekana kuwa hatari kwa waheshimiwa kuogopa kuumbuliwa mbele ya mahakama, kwanini mahakama isifanye hivyo kwa njia ya usiri?
Kinachofanyika ni ubaguzi wa wazi wazi wakati wa kushughulika na watu wanaotuhumiwa kwa makosa ya jinai.
Kanuni ya adhabu iko wazi kuwa kila mtu anayetenda kosa la jinai, lazima afikishwe mahakamani na si kwenye kamati.
Kama watawala wetu wameamua kuvunja sheria na kubagua wananchi ili kuwalinda wenzao, kwanini isiundwe tume inayohusisha watu wenye udhu kama vile majaji au Watanzania wanaoaminika na kujulikana kwa udhu na uzalendo wao badala ya hii danganya toto?
Hakuna haja ya kufikiria juu ya heshima ya wabunge ingawa wakishajihusisha na rushwa heshima yao inapotea.
Kama siyo Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kutekwa na ofisi ya rais hadi ikapoteza maana kwa kuwa chombo cha kulinda na kusafisha mafisadi, ingeweza kufanya kazi ya kuwachunguza hata kuwashitaki watuhumiwa kama wangepatikana na mashtaka.
Lakini, kwa vile TAKUKURU haina heshima wala udhu tena, ingeundwa tume yenye kuwa huru na kuwachunguza hawa watuhumiwa.
Hebu fikiria. Watu wanatuhumiwa kwa rushwa na wanaendelea kukaa bungeni wakati walipaswa kuwajibishwa kungoja taarifa za uchunguzi. Hii pekee inatosha kuonesha kuwa haki haitatendeka.
Wabunge wanapotuhumiwa kula rushwa, kwa maana nyingine ni kwamba Bunge limetuhumiwa chini ya dhana ya uwajibikaji wa pamoja.
Hivyo, kuruhusu Bunge kuchunguza wabunge wake wanaotuhumiwa kula rushwa, ni sawa na kulifanya kuwa mtuhumiwa, mwendesha mashitaka, polisi mkamataji na hakimu katika kesi inayolikabili.
Hapa, haki haitatendeka zaidi ya kuvuruga mfumo mzima wa utawala wa sheria kama upo. Bunge linachukuliwa kama mtuhumiwa si kwa maana kuwa wabunge wote ni wala rushwa. Hasha. Linatuhumiwa kutokana na ubovu wa mfumo na muundo wake. Kama Watanzania na serikali pamoja na taasisi nyingine kama Bunge wanachukia rushwa, basi waache sheria ichukue mkondo wake katika kushughulikia wabunge wanaotuhumiwa kula rushwa.
Bila kufanya hivyo, umma utaona ni kama sanaa na viini macho kama kawaida. Itajenga picha kuwa wanaojidai wanapambana na rushwa ndio wala rushwa wenyewe.
Ni pigo kwa haki hasa pale watunga sheria wanapokuwa wala rushwa wenyewe. Hawa hawawezi kutunga sheria za kupambana na rushwa wala ufisadi kwa vile wananufaika na jinai hizi.
Inakuwaje watendaji wengine wakituhumiwa wanakamatwa na kuwekwa ndani huku wakipelekwa mahakamani moja kwa moja, lakini si kwa wabunge wanaopaswa kuwa mfano?
Je, wabunge wa namna hii wanaweza kutunga sheria za kupambana na kile wanachonufaika nacho?
Je, wabunge wa namna hii wakishirikiana na serikali inayotuhumiwa kupatikana kwa njia ya kuiba pesa ya umma na kutoa rushwa wanaweza kuivusha nchi yetu?
Rejea madai ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa, kuwa Rais Jakaya Kikwete aliingia madarakani kwa kutumia pesa ya wizi toka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu. Bahati mbaya, pamoja na kuchagizwa akanushe hata kutoa maelezo kuhusiana na tuhuma hizi, Kikwete siku zote amegwaya kufanya hivyo kwa kuchelea anaweza kuumbuliwa zaidi.
Tatu, kinachofanyika licha ya kuwa kiini macho na juhudi za kulindana, ni sawa na kupeleka kesi ya wizi wa mahindi inayomkabili ngedere kwa ngedere mwenzie au nyani. Hukumu yake inajulikana kuwa ngedere watashinda tu. Kwa vile mchezo wa mahakimu wao ni ule ule.
Kama upogo huu hautarekebishwa, kuna uwezekano wa wabunge wasiokula rushwa nao kuanza rushwa. Maana wanajua wakifichuliwa kesi yao itahukumiwa na wenzao tena wenye kukubuhu kwenye jinai hii.
Nne, wengi wa wajumbe ni wakereketwa na makada wa chama tawala ambacho kinajulikana kwa tabia yake ya kulindana.
Rejea maneno ya Mbunge Anne Kilango aliyekaririwa akisema kuwa wabunge wanapaswa kulinda maslahi ya chama badala ya maslahi ya nchi.
Alikaririwa akisema: “Tulimtosa Lowassa, baadaye ukweli umejulikana, na sasa makosa yetu yanaigharimu serikali na CCM. Tusirudie makosa yale yale, tuwaache hawa kwa maslahi ya CCM.”
Maneno haya ya kifisadi ya Kilango yanaonesha CCM ilivyodhamiria kulinda maslahi yake hata kwa kuhujumu taifa.
Hii ikichangiwa na baadhi ya wanakamati kupata ubunge wao baada ya kushindwa, lazima watalipa fadhila kwa chama kilichowawezesha.
Nani mara hii kasahau jinsi mjumbe mmojawapo, Gosbert Blandes alivyotuhumiwa kupewa ushindi wa ubunge mezani kutokana na mchezo mchafu wa kuchakachua matokeo?
Blandes pia alituhumiwa kutoa hongo kwenye uchaguzi ukiachia mbali kutokuwa na udhu wa kutosha zaidi ya kupaswa kuchunguzwa yeye mwenyewe. Wajumbe kama Brigedia mstaafu Hassan Ngwilizi hawawezi kutenda haki ikizingatiwa kuwa ni wakereketwa wa CCM.
Wajumbe kama John Chiligati wanajulikana walivyo na mamlaka chamani ukiachia mbali mjumbe kama Riziki Omar Juma kutoka kwenye chama chenye ushirikiano na CCM.
Tumalizie kwa kuwasihi Watanzania wakatae huu usanii na ushirika katika ufisadi unaofanywa na taasisi zinazojiita zao wakati si zao, bali za kikundi kidogo cha watu kilichojihalalishia ulaji kwa gharama zao. Kundi lililowageuza wanachi punda wa kubeba mizigo yake.
Swali kuu la kujiuliza hapa ni je, Spika wa Bunge, Anna Makinda, Bunge na wabunge wanataka kumdanganya nani kuwa wanaweza kutuhumiwa, wakajichunguza au kuchunguzana na kuhukumiani kwa haki?

Lowassa: Tuko tayari kwa vita

Lowassa: Tuko tayari kwa vita
•  Asema jeshi liko tayari kiakili kuingia vitani na Malawi


KAMATI ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, imesema majeshi ya Tanzania yapo tayari kiakili na kivifaa ikibidi kuingia vitani kutokana na mzozo wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Edward Lowassa alipozungumza na waandishi na habari na kusisitiza Tanzania inaomba isifike katika hatua hiyo, lakini ikibidi wanajeshi wetu wapo imara kutetea mipaka ya nchi hadi tone lao la mwisho la damu.
“Jeshi letu lipo tayari, na tumeridhika na utayari wao na ‘commitment’ yao. Sisi ni moja ya jeshi lililojiandaa vizuri sana na miongoni mwa majeshi mazuri duniani. Tunajivunia vijana wa Tanzania waliopo kwenye jeshi letu. Tupo imara kiakili, vifaa vya kisasa,” alisema.
Alisema kamati hiyo inaunga mkono kauli ya serikali iliyotolewa juzi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, kwani ni sahihi inayoelezea msimamo wa Tanzania kuhusu jambo hilo.
Alisema kuwa wanategemea jambo hilo litamalizika kidiplomasia ndani kwa ndani ama ikibidi kuomba msaada wa watu wengine kusuluhisha kwa kuwa Tanzania na Malawi ni marafiki na ndugu.
“Watu waliopo mipakani ni ndugu, tusingependa kufika mahali kutokuelewana mpaka kuhusisha vyombo vya ulinzi na usalama, lakini kwa faida ya Watanzania tumepewa maelezo ya jeshi letu, tumeridhika kwamba ikibidi jeshi letu limejipanga vizuri sana.
“Watanzania wasiwe na shaka yoyote, wanajeshi wamejipanga vizuri na kwa uhakika na kama ilivyo ahadi yao, wapo tayari kulinda nchi yetu mpaka tone la mwisho la damu yao,” alisema na kuongeza kuwa kama wabunge, nao wameridhika na maandalizi ya jeshi, kwani wapo imara na timamu.
Alisema serikali haitaki kufika huko, kwani wakati wa Vita ya Uganda mwaka 1978, wananchi waliumia na kwamba kama nchi, inafahamu athari za vita kiuchumi na kwa maisha ya binadamu.
“Hatutaki kufika huko kwani si jambo jema, ndiyo maana tunasema tumalize kwa njia ya mashirikiano na kwa mazungumzo ya kidiplomasia ya mawaziri wanaohusika ikishindikana tutafute msuluhishi,” alisema.
Mwaka 1978, Tanzania iliwahi kuingia katika vita na Uganda, baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Iddi Amin Dada, kuvamia sehemu ya Tanzania na kudai kuwa ni yao.
Juzi, Membe alitoa tamko la serikali na kuyataka makampuni yote yanayoendelea kufanya utafiti wa mafuta katika ziwa hilo kuondoka mara moja pamoja na Serikali ya Malawi kuheshimu mazungumzo yaliyofikiwa. Alisisitiza eneo linalobishaniwa katika ziwa hilo lipo Tanzania.
Alisema pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuzipiga marufuku ndege za utafiti za kampuni hizo, bado zilikaidi na ndege tano zilitua katika eneo la Ziwa Nyasa.
“Serikali ya Tanzania inapenda kuzionya na kuzitaka kampuni zote zinazoendelea na shughuli za utafiti katika eneo hilo zisitishe mara moja kuanzia leo Jumatatu,” alisema Membe na kuongeza kuwa, Serikali ya Tanzania iko tayari kulinda mipaka yake kwa gharama yoyote.
Alisema kwa kuzingatia nyaraka zilizotengenezwa na wakoloni wa Kiingereza mwaka 1928 na 1938, zinaonesha kuwa mpaka wa ziwa hilo upo katikati.
Alisema hoja ya Tanzania ina nguvu kulingana na sheria za kimataifa kwa vile tatizo kama hilo linafanana na mgogoro uliokuwepo kati ya Cameroon na Nigeria.

Kipigo cha Dk. Ulimboka chazua balaa Tigo

Kipigo cha Dk. Ulimboka chazua balaa Tigo
•  Wafanyakazi 30 watimuliwa wakidaiwa kutoa mawasiliano ya siri kwa Gazeti la MwanaHalisi


KUTEKWA, kupigwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Chama cha Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka na hatimaye kufungiwa kwa Gazeti la MwanaHalisi kwa muda usiojulikana, kumeleta kizaazaa katika kampuni ya simu za mkononi ya Tigo, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Habari kutoka ndani ya kampuni hiyo ya simu yenye mtandao mpana nchini, zinasema kuwa zaidi ya wafanyakazi 30 wamefukuzwa kazi na wengine wako kwenye uchunguzi wakituhumiwa kuvujisha mawasilino ya siri ya simu za wateja kwa Gazeti la MwanaHalisi.
Kwa mujibu wa habari hizo, taarifa za mawasiliano za simu zinazodaiwa kuvujishwa na wafanyakazi hao, zilikuwa kati ya Dk. Ulimboka, Afisa Usalama wa Ikulu na watu aliowasiliana nao kabla ya kutekwa.
Rais Jakaya Kikwete amepata kuliambia taifa mara mbili kwa njia ya televisheni, mwishoni mwa Juni na alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari wiki iliyopita, kwamba serikali yake haihusiki kuteka, kutesa na kumtupa daktari huyo porini.
Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda amepata kuliambia Bunge kuwa, serikali yake haihusiki na utekaji, utesaji na kuhoji, “...serikali imteke ili iweje?”
Hivi karibuni serikali ililifungia Gazeti la MwanaHalisi baada ya kuandika habari iliyomtaja ofisa mmoja wa Idara ya Usalama wa Taifa Ikulu (TISS), kuwa ndiye aliyetekeleza mpango wa kumteka, kumpiga na kumtesa hadi kumjeruhi Dk. Ulimboka, ambaye kwa sasa anaendelea na matibabu kwenye hospitali moja nchini Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa habari hiyo ambayo serikali inadai kuwa ni ya uchochezi, MwanaHalisi ilianika namba ya simu ya ofisa huyo pamoja na watu wengine wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo linaloendelea kuchunguzwa na kamati maalumu iliyoundwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Vyanzo vya habari kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi waliokumbwa na sekeseke hilo, zinasema kuwa waliofukuzwa wengi ni wafanyakazi wa kitengo cha IT ambao wanadaiwa kuhusika kutoa taarifa za siri ya mawasilino kati ya Dk. Ulimboka na watu wanaoaminika kuwa ni wabaya wake.
Mmoja wa wafanyakazi kutoka Kampuni ya Tigo, aliliambia gazeti hili kuwa mbali na kutuhumiwa kutoa siri kwa Gazeti la MwanaHalisi, wafanyakazi wengine wametimuliwa kwa madai ya kufanya udanganyifu kwenye huduma za Tigo Pesa na kujipatia fedha.
“Kweli watu wengi wamefukuzwa wakituhumiwa kutoa siri kwa Gazeti la MwanaHalisi, lakini wengine walikuwa wakishirikiana na mawakala wa Tigo Pesa kuiibia kampuni.
“Kwa mfano mfanyakazi alikuwa anakubaliana na wakala kumwingizia kiasi kama cha sh milioni moja, lakini anaweza kuingiza hadi sh milioni 1.5 na kati ya hizo sh 500,000 ni mali yake,” alisema mfanyakazi huyo.
Akizungumzia na Tanzania Daima Jumatano, Mhariri Mkuu wa Gazeti la MwanaHalisi, Jabir Idrissa alishangazwa na taarifa za Tigo kuwafukuza wafanyakazi wake kwa sababu ya habari iliyochapishwa na gazeti lake.
“Chanzo chetu cha habari hakikutoka kwa wafanyakazi wa Tigo. Kama wamefukuzwa kwa sababu ya MwanaHalisi, wamewaonea bure. Kama Tigo ndio waliotupa taarifa na zile za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), zilitoka wapi?” alihoji Jabir na kusisitiza wafanyakazi hao wameonewa bure.
Ofisa Uhusiano wa Tigo, Edward Shila, alipohojiwa kuzungumzia tukio hilo, hakukubali wala kukataa madai hayo na kumtaka mwandishi kumtumia maswali kupitia e-mail yake ili aweze kuyatolea majibu kiofisi.
“Kama una maswali naomba uniandikie kupitia e-mail yangu ambayo nakutumia sasa hivi…maana siko tayari kutoa kauli yoyote isiyokuwa ya kiofisi,” alisema.
Naye Omary Matulla ambaye amejitambulisha kuwa ni ofisa wa kitengo cha kumbukumbu katika kampuni hiyo, alikanusha kuwapo kwa taarifa za kufukuzwa wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Alisema kuwa kila mfanyakazi ana mipaka ya kufanya kazi katika kampuni hiyo, na pia ni wajibu wa kila mtumishi kutunza siri kubwa.
“MwanaHalisi ana mbinu zake za kupata habari wala haiwezekani kupata habari kupitia kampuni yetu na hata hivyo jambo hilo si rahisi hata kidogo kutokea,” alikanusha Omary.
Dk. Ulimboka alitekwa usiku wa Juni 26, kusukumizwa kwenye gari, kupigwa, kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa kucha na kutolewa meno na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Tangu kutokea kwa tukio la kutekwa kwa Dk. Ulimboka, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu, wamekuwa wakiinyoshea kidole serikali kwamba ndiyo iliyohusika.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi mkoani Dar es Salaam, Suleiman Kova, hivi karibuni alitangaza kumfikisha mahakamani mtu mmoja aliyedai kukiri kuhusika na utekaji wa Dk. Ulimboka.
Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa, polisi wamekamata mtu aitwaye Joshua Malundi kutoka Kenya ambaye amekiri kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka.
Alidai kuwa mtuhumiwa alikwenda kutubu katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, Kawe, Dar es Salaam.
Lakini hata hivyo, mchungaji wa kanisa hilo, Josephat Gwajima alikana kauli ya Kova juu ya mtuhumiwa huyo, akisema hajakwenda kutubu kwao.

Friday, August 3, 2012

Mrisho Ngasa auzwa Simba kama kifurushi



HATIMAYE mshambuliaji Mrisho Ngassa wa timu ya Azam FC, amepelekwa Simba kwa kitita cha sh mil. 25, kiasi ambacho kimeafikiwa na klabu yake iliyomsajili msimu wa 2009/10 kutoka Yanga kwa dau la sh mil. 59.
Habari zilizoifikia Tanzania Daima jana jioni, zilisema kuwa suala hilo limefanyika baada ya kikao cha pamoja kati ya Azam na Simba kilichofanyika jana.
Simba imemtwaa nyota huyo siku moja tu tangu uongozi wa Azam umweke sokoni kwa sh mil. 50, wakikerwa na mchezaji huyo kuonesha mapenzi yake kwa timu yake ya zamani ya Yanga.
Habari za awali ambazo ziliifikia Tanzania Daima, zilisema licha ya Azam kuweka dau hilo, hadi jana mchana timu za Simba na Yanga, zilikuwa tayari kumsajili kwa dau tofauti.
Wakati Yanga wakitenga kiasi cha shilingi mil. 20 kumrejesha nyota huyo kundini, Simba wao wapo tayari kutoa kiasi cha sh mil. 25 kwa ajili ya kuichezea kwa miaka miwili.
Kabla ya kwenda mitamboni, Meneja wa Azam FC, Patrick Kahemele, kupitia mtandao wa kijamii, alikiri klabu za Simba na Yanga kumtaka, pia zikitofautiana kwa dau.
“Hadi hivi sasa ofa ya Simba ni sh mil. 25 na Yanga sh mil. 20. Kutokana na hilo, Simba wapo kwenye nafasi kubwa ya kumnyakua Ngasa (Mrisho). Kesho (leo) ni siku ya mwisho. Ingawa tungependa kumuuza Yanga, lakini tutampeleka kwa timu yenye ofa nzuri zaidi,” alisema Kahemele na kusisitiza.
“Lengo la Azam lilikuwa ni kumpeleka Mrisho kwenye timu ambayo atacheza kwa raha na amani, kutokana na yeye kuivaa na kuibusu jezi ya Yanga siku ambayo Azam FC haikuwa na mchezo na Yanga….. Azam FC inaamini kuwa Yanga ilikuwa sehemu sahihi kwa Mrisho, lakini uongozi wa Yanga umeonekana kutokuwa na haja naye, ndiyo maana umeonekana kukataa kutoa ofa ya maana.
“Kutokana na sababu hizo, Azam FC italazimika kumuuza Simba, kwani hatuhitaji kuwa na mchezaji ambaye anafanya vitendo vya kuidharau ‘brand’ ya Azam FC ambayo tunajaribu kuijenga,” alisema Kahemele.
Kitendo cha Azam kuamua kumuuza nyota huyo Simba kwa kigezo tu cha dau kubwa bila kuzingatia mapenzi ya mchezaji, hakina tofauti ya mchezaji huyo kuuzwa kama kifurushi ambacho mwelekeo wake hutegemea matakwa ya mbebaji.
Juhudi za kumtafuta nyota huyo kupata msimamo wake juu ya maamuzi hayo yaliyofanywa na Azam na Simba, jana ziligonga ukuta kwani simu yake ilikuwa haipo hewani.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wachezaji wa timu ya Azam wamesikitishwa na kitendo cha klabu hiyo kumtimua Kocha Mkuu, Stewart Hall, wakisema ni kati ya makocha bora, hivyo uamuzi wa kumfukuza si sahihi.
Kauli ya wachezaji hao inatokana na kocha huyo kuipatia mafanikio makubwa timu hiyo ikiwamo kuiwezesha kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Bara, pia nafasi ya pili kwenye michuano ya Kombe la Kagame nyuma ya Yanga, licha ya kushiriki mara ya kwanza.

CHADEMA waitaka CCM kuvunja Bunge


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wake kulivunja Bunge ikiwa kina ujasiri, uzalendo na uadilifu ili kuwezesha mabadiliko ya mfumo wa utawala.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari akielezea kauli ya CCM iliyotolewa na Katibu wake wa Itikadi na Uenez Nape Nnauye na kusema inapaswa kuwa katika vitendo zaidi kwa kuwavua uanachama viongozi waliotuhumiwa kwa ufisadi tangu mwaka 2007.
“CHADEMA kinaukumbusha umma kauli ya Mwalimu Nyerere kwamba chama legelege, huzaa serikali legelege, matokeo ya hali hiyo ni kuwa Bunge legelege, hali hii inajidhihirisha kwa CCM kushindwa kushughulikia tuhuma za ufisadi dhidi ya viongozi wake ndani ya chama, Serikali na Bunge hali inayoathiri uwezo na uadilifu wa vyombo vya uchunguzi na kuchukua hatua zinazostahili,” alisema Mnyika.
Alisema CCM imeshindwa kusimamia misingi ya kupambana na rushwa kwa kutumia wingi wa wabunge wake kupitisha baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi nchini kuwa viongozi wa kamati muhimu za Bunge na kuwataja baadhi yao kuwa ni Kamati ya Mambo ya nje, Ulinzi na Usalama ambayo mwenyekiti wake ni Edward Lowassa na Kamati ya Fedha na Uchumi, mwenyekiti wake ni Andrew Chenge.
Mnyika pia aliutaka umma upuuzie kauli ya CCM ya kulipongeza Bunge kwa kusimamia rasilimali za nchi na kuhakikisha nchi inapiga hatua kimaendeleo, badala yake CHADEMA itaanza kuunganisha nguvu ya umma kutaka kamati zote za Bunge zivunjwe na kuundwa upya ili kuurejesha mhimili huo kwenye mwelekeo unaostahili.

CWT yaliponda Bunge, Serikali

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimelishutumu Bunge na Serikali kwa kuiingilia uhuru wa Mahakama kwa matamko yao kuwa mgomo wa walimu unaoendelea hivi sasa nchini ni batili.
Chama hicho pia kimelaani ufujaji wa fedha za umma unaofanywa na watendaji wa serikali kwa kutoa matangazo katika vyombo vya habari yanayoelezea kuwa mgomo huo si halali.
Rais wa CWT, Gratian Mukoba, ndiye aliyetoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kuelezea mgomo, vitisho na kukamatwa kwa baadhi ya walimu wanaoutekeleza.
Mukoba alisema mgomo wao ulizingatia kifungu cha 80(1) cha sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004, hali iliyoifanya serikali kukimbilia mahakamani kwa lengo la kuomba mahakama kutoa zuio kwa CWT kutoendelea na mgomo huo.
Alisema wakati suala hilo likiwa mahakamani na kabla halijaamriwa serikali kupitia kwa watendaji wake, akiwamo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiq, wakaingilia uhuru wa mhimili mwingine kwa kuutangazia umma kuwa mgomo ni batili.
“Tumesikitishwa kuona Bunge lenye dhamana ya kuisimamia serikali nalo limeamua kuingilia uhuru wa mahakama kwa lengo la kuisaidia serikali pale Naibu Spika, Job Ndugai, alipoitangazia jamii kuwa mahakama ingetoa hukumu Julai 31, saa saba mchana wakati pande zote mbili zilikuwa hazijasikilizwa,” alisema.
Vitisho, kukamatwa
Akizungumzia vitisho na kukamatwa kwa walimu walio katika mgomo, Mukoba alisema tayari wamepokea taarifa za sehemu mbalimbali kuwa walimu wanakamatwa na kulazimishwa kufundisha, hili si jambo jema.
Alitaja baadhi ya mikoa inayofanya vitendo hivyo kwa walimu ni Pwani, Morogoro na Ruvuma ambapo viongozi na watendaji wa CWT wanapewa vitisho na wakuu wa mikoa pamoja na kamati za ulinzi za mikoa.
Alisema katika wilaya za Tarime, Rungwe, Kyela na Babati viongozi wa CWT wameshakamatwa huku mkoani Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa huo, Sadik amewatisha wanachama na viongozi huku akiamrisha wakamatwe.
Mukoba alisema Sadiq ameudanganya umma kuwa yeye (Mukoba) aliripoti katika kituo chake cha kazi ambacho ni Shule ya Benjamin Mkapa na kusaini daftari la mahudhurio lakini baadaye alianza kuwazuia wenzake wasiende kazini.
Aliongeza kuwa taarifa hiyo ya mkuu huyo wa mkoa imelenga kumchafulia jina ili aonekane msaliti mbele ya jamii na hasa walimu ambao sasa wanaendelea na mgomo kudai haki zao.
Hali ya mgomo
Mukoba alisema hadi sasa walimu wamegoma kwa asilimia 95 na wameshindwa kufikia asilimia 100 kwa kuwa kila sehemu kuna wasaliti ambao wakati mwingine hawana nia hiyo bali wamezaliwa waoga wa kupigania masilahi yao.
“Tunajua wapo wanaoshindwa kusimamia haki yao kwa dhana ya kujipendekeza ili wafikiriwe katika madaraka mengine, wengine hawaoni mbele na pia wapo wasaliti na hawa hawakosekani kwani walikuwapo hata enzi ya mitume,” aliongeza Mukoba.
Mukoba alitoa wito kwa serikali kuwaachia huru walimu wote waliokamatwa na badala yake itafute njia sahihi ya kutatua tatizo kwa kuwa suala hilo lipo mikononi mwao.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona serikali ikifunga milango kwa ajili ya kukutana na walimu na badala yake ikidhani njia ya mabavu ndiyo suluhisho la kumaliza mgogoro huo.

Kikwete amsafisha Chenge



•  Asema hakuna rushwa kwenye kashfa ya rada


RAIS Jakaya Kikwete amevunja ukimya kwa kusema kwamba hakuna rushwa kwenye kashfa ya ununuzi wa rada kutoka nchini Uingereza.
Ingawa Rais Kikwete hakutaja jina, lakini kwa kauli hiyo ni dhahiri kwamba amemsafisha Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge (CCM), ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitajwa ndani na nje ya chama chake kuhusika na kashfa ya ununuzi wa rada kutoka Kampuni ya BAE- System.
Chenge, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, anatajwa kuhusika kutoa ushauri wa kisheria wakati huo akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ushauri ambao unatajwa kuzingatiwa katika hatua za uamuzi.
Mwingine anayehusishwa na kashfa hiyo ni aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT) Dk. Idriss Rashid.
Pamoja na hao, wanatajwa wafanyabiashara wenye asili ya India, lakini ambao wanaishi/walipata kuishi Tanzania, Tanil Somaiya, ambaye alikuwa akimiliki kampuni ya uwakala wa simu ya Shivacom na Sailesh (Shailesh) Vithlani kuwa watu wa kati wa biashara hiyo.
Akijibu swali kutoka kwa mmoja wa wahariri aliyetaka kujua hatua zilizochukuliwa kwa waliohusika na ununuzi wa rada wakati chenji yake imesharejeshwa, Rais Kikwete alisema Serikali ya Uingereza iliyokuwa ikichunguza kashfa hiyo imebaini kuwa hakukuwa na rushwa katika ununuzi wa rushwa.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, uchunguzi wa Serikali ya Uingereza ulibaini kuwa kulikuwa na makosa ya uchapaji, lakini hakuna mtu aliyehusika kutoa wala kupokea rushwa.
“Kama Uingereza waliochunguza kashfa hiyo wamefika mahala wanasema kulikuwa na makosa ya uchapaji tu, mtu wenu mnamfikisha mahakamani kwa ushahidi upi?” alihoji Rais Kikwete.
Mchakato wa ununuzi wa rada, uliwahusisha watu wa madaraka na kada mbalimbali ambao ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair.
Blair anatajwa kuwa ndiye aliyemshawishi aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo, Benjamin Mkapa, kununua rada hiyo kutoka Kampuni ya kutengeneza silaha ya Uingereza BAE-Systems. Wakati huo aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa, Clare Short, alikataa katakata Tanzania, moja kati ya nchi masikini kabisa duniani, kutumia sh bilioni 40 kununua rada katikati ya umasikini unaonuka.
Hata hivyo chenji hiyo ya rada, zaidi ya sh bilioni 75 zimerejeshwa nchini baada ya hati ya makubaliano baina ya pande zinazohusika kusainiwa.
Hati hiyo ilisainiwa kati ya Serikali ya Tanzania, Kampuni ya Uuzaji wa Silaha ya Uingereza (BAE - System), Ofisi ya Uingereza ya Kupambana na Ufisadi (SFO) na Idara ya Kimataifa ya Misaada ya Maendeleo (DFID).
Chenge mwenyewe huko nyuma alipata kuzungumzia suala hilo na hasa, kumiliki kwake kwa akaunti ya fedha nyingi nje ya nchi inayohusishwa na mlungula wa ununuzi wa rada.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Edward Hosea, alipata mara mbili kunukuliwa akisema Chenge hakuwa na kesi ya kujibu katika kashfa hiyo ya rada.
Kuhusu sakata la wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), iliyohusisha Kampuni ya Kagoda iliyochota sh bilioni 40, Rais Kikwete alisema suala haliko kwake bali mikononi mwa vyombo vya dola.
“Hili la Kagoda liko mikononi mwa vyombo vya dola, wanaendelee nalo,” alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo Rais Kikwete alitamba kuwa serikali yake imejitahidi sana kupambana na rushwa kwa kuimarisha uwezo wa TAKUKURU.

Zitto ajibu mapigo



•  Akana kuhongwa, adai ni mkakati wa CCM kujitakasa


NAIBU Katibu Mkuu wa CHADEMA na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, amesema tuhuma za rushwa zinazoelekezwa kwake ni mkakati wa makusudi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutaka kuaminisha wananchi kuwa ufisadi upo pia ndani ya upinzani.
Zitto amedai kuwa kwa bahati mbaya pasipo kujua wako baadhi ya wabunge wa upinzani nao wameingia kwenye mtego huo wa uzushi wa CCM bila tahadhari kuwa hiyo ni vita ya kisiasa ya kuisambaratisha CHADEMA.
Mbunge huyo alifichua mbinu hizo jana mjini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuelezea hatua ya tuhuma za rushwa zilizotolewa kwenye majadiliano ya Wizara ya Nishati na Madini.
“Nalazimika kukutana nanyi kutoa maelezo juu ya tuhuma zenye shinikizo la kisiasa zinazoelekezwa kwangu binafsi kwamba hata mimi nimeshiriki katika vitendo vya rushwa, kwa nafasi yangu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC). Taarifa hizo, kama kawaida ya uzushi mwingine wowote zimesambazwa kimkakati na kwa kasi kubwa kiasi cha kuukanganya umma,” alisema.
Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema anawajibika kuwatoa hofu wananchi kutokana na hisia potofu kwa vile ana dhamana kubwa ya uongozi.
“Mkakati huo wa kuniunganisha na baadhi ya wabunge wanaotuhumiwa kwa kupokea rushwa unatekelezwa na watendaji wa serikali ambao wamekuwa wakizieneza habari hizo na hususan kutoa taswira kwamba baadhi ya kauli zangu zinatokana na ushawishi wa rushwa,” alisema.
Alisema kuwa watu mbalimbali wamefikia kuaminishwa habari hizo kiasi cha wengine kuuliza kwanini hakutajwa katika orodha iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu, alipowataja wabunge sita wa CCM wanaotuhumiwa kwa rushwa.
Zitto ambaye aliongozana na wabunge 14 wa CHADEMA katika mkutano huo, alisema kuwa hiki ni kipindi cha pili cha ubunge na akiwa mwenyekiti wa POAC, ukiwa ni takriban mwaka wa saba sasa, kwamba kamati yake inasimamia mashirika 259 ya Umma na si TANESCO peke yake.
“Zipo hoja pandikizi za kutaka POAC ivunjwe na hasa zikinilenga mimi binafsi. Nafahamu kiu ya wasioitakia mema nchi yetu kuiona POAC ikivunjwa au sura zikibadilishwa, kwa kuwa kamati hii imekuwa mwiba kwa mikakati yao ya kifisadi,” alisema.
“Mimi Zitto Zuberi Kabwe sina bei, sijawahi kuwa nayo na sitarajii kuwa nayo huko mbeleni. Daima nimesimamia kidete maadili ya uongozi bora katika maisha yangu yote ya siasa, na nawaahidi sitarudi nyuma katika mapambano dhidi ya rushwa katika nchi hii pamoja na mikakati ya aina hii ya kunidhoofisha na kunivunja moyo,” alisema.
Aliweka bayana kuwa kwa maoni yake POAC isihusishwe na tuhuma hizo kwa vyovyote vile kwamba yuko tayari ahukumiwe yeye na si kuhusisha wajumbe wengine ambao hawatajwi mahala popote katika tuhuma hizo mbaya katika historia ya Bunge.
“Nitakuwa tayari kuinusuru POAC na masilahi ya taifa letu kwa kujiuzulu uenyekiti iwapo itathibitika pasipo shaka kuwa nimehongwa. Kamati ya POAC ni muhimu zaidi kuliko mimi,” alisema mbunge huyo.
Zitto alisema anafahamu kwamba kuna wanasiasa hasa wa upinzani ambao wanautaka sana uenyekiti wa POAC na wanafanya kila njia kutaka kuidhoofisha, lakini wanashindwa kuelewa kuwa anayepanga wajumbe wa kamati ni Spika wa Bunge.
“Msishangae pia kuja baadaye kubaini kwamba baadhi ya wanasiasa wenye midomo mikubwa ya kutuhumu wenzao wao ndio vinara wa kupokea rushwa,” aliongeza.
Zitto alisema baada ya bodi ya wakurugenzi ya TANESCO chini ya uenyekiti wa Meja Jenerali mstaafu Robert Mboma, kutangaza kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu, William Mhando, ili kupisha uchunguzi, POAC ilimuandikia Spika kumuomba aridhie kuwaita Bodi ya TANESCO, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na pia Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kujiridhisha na tuhuma zote zinazotajwa zifanyiwe uchunguzi wa kina na hatua kuchukuliwa.
“Tulifanya hivyo kwani kulikuwa na tetesi kuwa kusimamishwa kazi kwa Mhando siku chache kabla ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kulikuwa na lengo la kufunika ‘madudu’ makubwa zaidi kwa kulichagiza Bunge na tukio hilo dogo, mkakati ambao naona umefanikiwa sana,” alisema.
Zitto alisema kuwa kitendo hicho cha halali na kwa mujibu wa kanuni kilichofanywa na kamati yake kimetafsiriwa kwa makusudi na baadhi ya watu kwamba ni ishara ya kuwa yeye ana masilahi binafsi na TANESCO na hususan Mhando.
“Baada ya tukio hilo, nikiwa hapa Dodoma, mwandishi wa habari wa gazeti moja alinifuata akiniambia kuwa wamekutana na Waziri Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliachim Maswi, hapa bungeni na wamewaambia kuwa mimi nimepewa rushwa. Hakutaja nimepewa rushwa na nani, kiasi gani na wala kwa lengo gani,” alitanabaisha.
Aliongeza kuwa alijaribu kumtafuta kwa simu Waziri Muhongo na Maswi ili wampe ufafanuzi juu ya yeye na kamati ya POAC kuhusishwa na tuhuma hizo bila mafanikio, hali ambayo alidai inamwondolea mashaka juu ya ushiriki wao katika kueneza au kuthibitisha uvumi huo.
“Binafsi sijawahi kuwa na mawasiliano ya aina yoyote na uongozi wa TANESCO kushawishiwa juu ya hatua ambazo POAC ndio imezichukua za kutaka kujiridhisha juu ya utaratibu uliotumika,” alisema.
Alibainisha kuwa hakuna wakati wowote, popote ambapo yeye binafsi au kamati yao imekataa Mhando kuchunguzwa kwa tuhuma zozote kwamba wanachosisitiza wakati wote ni ufuatwaji wa taratibu, kanuni na sheria, jambo alilodai atalisimamia, iwe masika au kiangazi.
Zitto alisema ni kwa sababu hiyo, amekutana na Spika Anne Makinda na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, juzi na kwamba kwa kujiamini kabisa amewaomba suala la tuhuma za rushwa zinazotajwa dhidi yake zichunguzwe na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kina.
“Nimekwenda mbali zaidi kukiomba chama changu CHADEMA kifanye pia uchunguzi na tathmini yake kwa kina kujiridhisha na tuhuma hizo, natumia fursa hii pia kuomba vyombo vya dola vichunguze tuhuma hizo kwa nafasi yake ili kuweza kupata ukweli.
Zitto alisisitiza kuwa lazima wafike mahali kama viongozi kwamba utaratibu unapokiukwa na yeyote yule, au uongo unapotolewa hadharani waseme bila kuogopa.
Alisema kuwa kwa imani hiyo, hatasalimu amri mbele ya dhamira zao ovu hata atakapobaki peke yake katika mapambano hayo ya kulinda na kutetea rasilimali za taifa zinufaishe Watanzania wote.
Alimtaka Waziri Muhongo kuwaeleza ukweli wananchi kuwa ili mgawo wa umeme usiwepo tena nchini serikali itapaswa kulipa sh bilioni 42 kila mwezi kwa kampuni binafsi za kufua umeme za IPTL na Symbion, ukweli ambao alidai utakuja kujulikana wenyewe muda si mrefu.