|
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)
imetangaza bei kikomo ya bidhaa za mafuta ya petroli nchini ambayo
imeongezeka kwa sh 70 kwa lita sawa na asilimia 3.4.
Hatua hiyo ni wazi kuwa itasababisha gharama za nauli kuwa juu, pamoja
na usumbufu kwa abiria katika nyakati hizi za kuelekea sikukuu za
Krismasi na Mwaka Mpya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Anastas Mbalawa kwa niaba ya
Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Haruna Masebu, alisema kuwa bei hizo
zitaanza kutumika kuanzia leo na kuwataka wamiliki wa vituo vya mafuta
kutambua bei kikomo ya bidhaa hizo.
Taarifa hiyo ilitaja bei hizo katika Jiji la Dar es Salaam kwa petroli
itakuwa sh 2,119, dizeli sh 1,999 na mafuta ya taa sh 2,023; Arusha
petroli sh 2,203, dizeli sh 2,083 na mafuta ya taa sh 2,107 huku Dodoma
petroli itauzwa sh 2,146, dizeli sh 2,058 na mafuta ya taa sh 2,082.
Mkoani Iringa petroli itauzwa kwa sh 2,183, dizeli sh 2,063 na mafuta
ya taa sh 2,087, huku Morogoro petroli itauzwa kwa sh 2,144, dizeli sh
2,024 na mafuta ya taa sh 2,048 na Bukoba petroli sh 2,334, dizeli sh
2,214 na mafuta ya taa sh 2,238.
Alisema kuwa bei za jumla na rejareja kwa mafuta aina zote ya petroli,
dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka ikilinganishwa na toleo lililopita
la Novemba 7, 2012.
“Katika toleo hili, bei za rejareja kwa dizeli imeongezeka sh 10 kwa
lita sawa na asilimia 0.53, bei ya mafuta ya taa imepungua kwa sh 3 kwa
lita sawa na asilimia 0.1, huku bei za jumla kwa kulinganisha matoleo
haya mawili zimeongezeka petroli kwa sh 69.56 kwa lita sawa na asilimia
3.52; dizeli kwa sh 10.04 kwa lita sawa na asilimia 0.52,” alisema.
Alisema kuwa bei ya mafuta ya taa imepungua kwa sh 3 kwa lita sawa na
asilimia 0.15 huku akisema kuwa mabadiliko ya bei hizo yametokana na
ongezeko la bei ya mafuta katika soko la dunia na kushuka kidogo kwa
thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani.
Mbalawa alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya mafuta ya mwaka 2008, bei
za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko ambapo
EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo
za bidhaa hizo.
“Kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei
ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo (price cap)
kama ilivyokokotolewa na fomula mpya iliyopitishwa na mamlaka yetu na
kuchapwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 454 la Desemba 23, 2011,”
alisema.
Aidha, alisema kuwa ni muhimu vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za
bidhaa hizo katika mabango yanayoonekana, huku ikionyesha bei ya
mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na
kituo husika.
Alisema kuwa ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei
inayoonekana vizuri kwa wateja, na kwamba adhabu itatolewa kwa kituo
husika.
|
No comments:
Post a Comment