|
ALIYEKUWA Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), Godbles Lema,
amewasilisha sababu 18, kuiomba Mahakama ya Rufaa nchini, itengue hukumu
ya awali iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Aprili mwaka huu
ambayo ilifuta ubunge wake.
Ombi hilo liliwasilishwa mahakamani hapo jana na mawakili wa Lema,
Method Kimomogoro na Tundu Lissu ambao walidai kuwa hukumu hiyo
iliyotolewa na Jaji Gabriel Rwakibalila haina hadhi ya kuitwa hukumu.
Mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa linaloongozwa na
Jaji Natharia Salum Massati, wakili Kimomogoro, alieleza mahakama kuwa
rufaa ya mteja wake ina jumla ya sababu 18 za kupinga hukumu iliyotolewa
na Jaji Rwakibalila.
Katika hukumu yake iliyoibua mjadala mkubwa nchini Aprili mwaka huu,
Jaji Rwakibalila alimtia hatiani Lema kwa makosa ya kutoa lugha za
kumkashifu mgombea mwenzie, Dk. Batilda Buriani (CCM) na kumfungia
kutogombea ubunge kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo.
Alidai kuwa, Jaji Rwakibalila alijielekeza vibaya katika hukumu yake
alivyosema kuwa kesi za uchaguzi hazitawaliwi na kanuni za sheria za
Uingereza kwani kuna maamuzi ya kesi mbalimbali yaliyokwishatolewa na
Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu nchini na kuruhusu kesi za uchaguzi
ziamuliwe kwa kutumia kanuni na sheria za Uingereza.
Katika hoja ya pili, Kimomogoro alidai kuwa Jaji Rwakibalila
alijielekeza vibaya kuruhusu wajibu rufaa, wasitaje maneno kwenye hati
ya madai ambayo walidai ni maneno ya udhalilishaji wa kijinsia na dini
ambayo yanadaiwa kutolewa na Lema, kwenye mikutano ya kampeni dhidi ya
Dk. Burian.
Hoja nyingine ni kwamba hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kwamba
wajibu rufaa kama kweli waliandikishwa kupiga kura katika Jimbo la
Arusha Mjini mwaka 2010 au la.
Kwa mujibu wa wakili huyo, hoja nyingine ni kwamba Jaji Rwakibalila
alikosea kisheria kusema kuwa mtu yeyote akiwemo mpiga kura ana haki ya
kufungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo ambalo yeye ni
mpiga kura na kuongeza kuwa, wao wanaomba Mahakama ya Rufaa itamke kuwa
wajibu rufaa (wapiga kura wa Jimbo la Arusha waliofungua kesi ile),
hawana haki kisheria kufungua kesi ile ya kupinga ubunge wa Lema kwani
mwenye haki ya kufanya hivyo ni Dk. Batilda mwenyewe.
Aliongeza kuwa, mpiga kura yeyote hana haki ya kufungua kesi ya kupinga ubunge wa Arusha Mjini kwani haki zao hazikuvunjwa.
Aidha, katika hoja nyingine alidai kuwa Jaji Rwakibalila hakutumia
maamuzi ya kesi za Mahakama ya Rufaa wala vifungu vya sheria ambavyo
mawakili wa pande zote mbili waliziwasilisha mbele yake katika
majumuisho yao ya mwisho.
Alidai kuwa, maamuzi ya Mahakama ya Rufaa katika kesi zile
yalisisitiza kuwa lazima kesi ithibitishwe bila kuacha mashaka yoyote,
lakini katika hukumu ya Lema, Jaji Rwakibalila imeacha mashaka mengi,
ndiyo maana Lema anadai jaji huyo alikosea.
Baada ya wakili Kimomogoro kuwasilisha hoja hiyo iliyodai Jaji
Rwakibalila hakutumia maamuzi ya kesi zilizowasilishwa mbele yake na
mawakili wa pande mbili, Jaji Massati alisema si lazima jaji au hakimu
atumie kesi zilizowasilishwa mbele yake na mawakili katika kutoa uamuzi.
Hoja nyingine ni kwamba, hukumu ya Lema iliegemea katika ushahidi wa
mdomo tu bila kuwepo ushahidi wa kuunga mkono kwani mashahidi wa mjibu
rufaa, waliotoa ushahidi walidai walimsikia Lema katika mikutano ya
kampeni akitoa maneno ya kumdhalilisha na kumkashfu Dk. Batilda, lakini
walishindwa kuleta CD, mikanda ya video kuthibitisha.
“Tulimueleza Jaji Rwakibalila kuwa mashahidi wa wajibu rufaa
hawaaminiki na kwamba ushahidi wao ulikuwa wa mazingira, lakini jaji
katika hukumu yake hakuna sehemu aliyoonyesha kukubali wala kukataa hoja
yetu hii,” alidai wakili Kimomogoro.
Wakili huyo alidai pia Jaji Rwakibalila alikosea alivyosema Lema ana
bahati kwani hakukamatwa wala kushitakiwa kwa kutoa lugha za kashfa na
udhalilisha katika mikutano ya kampeni za uchaguzi wa mwaka 2010.
Kutokana na madai hayo, alidai kuwa Lema anaiomba Mahakama ya Rufaa
itamke kuwa Jaji Rwakibalila alitamka neno hilo kwa bahati mbaya na
kutamka kwake neno hilo ndiko kulikomsukuma kufikia uamuzi wa kumfungia
Lema asigombee kwa kipindi cha miaka mitano.
“Kwa hoja hizo tulizoziwasilisha hapo juu, tunaiomba Mahakama ya
Rufani nchini itengue hukumu ya Jaji Rwakibalila kwani haina vigezo wala
hadhi ya kuifanya iwe hukumu, na pia tunaiomba mahakama iwaamuru
wajibu rufaa walipe gharama za uendeshaji wa kesi hiyo tangu ilipoanza
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na sasa Mahakama ya Rufaa,” alidai wakili
Kimomogoro.
Kwa upande wake wakili wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa
Uchaguzi Jimbo la Uchaguzi, Timon Vitalis, alidai kuwa sheria ya
uchaguzi haiwaruhusu wapiga kura kufungua kesi ya kupinga ubunge wala
wagombea ubunge, udiwani kwani aliyepaswa kufungua kesi hiyo ni Dk.
Batilda na siyo wajibu rufaa ambao ni wapiga kura wa Jimbo la Arusha
Mjini.
Hata hivyo hoja hizo zilipanguliwa na mawakili wa wajibu rufaa, Aluthe
Mugwai na Modest Akida na Wakili wa Msimamizi wa Uchaguzi na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Vitalis.
Mugwai na Akida walitetea kuwa hukumu ile ni sahihi na haistahili
kutenguliwa kwani imekidhi matakwa ya kisheria na kuomba mahakama hiyo
itupilie mbali rufaa ya Lema.
Mugwai alisema mawakili wa Lema wanaipotosha mahakama kwa kusema
hakukuwa na uthibitisho wowote ulioonyesha wajibu rufaa walikuwa wapiga
kura wa Jimbo la Arusha Mjini wakati ukurasa wa 10 katika hukumu
inayopingwa, inaonyesha namba za vitambulisho vya wapiga kura ambavyo ni
vya wajibu rufaa na wakati vikitolewa mahakamani, mawakili hao wa Lema
walikuwepo.
Kuhusu hoja ya jaji kwamba alijielekeza vibaya kusema kuwa sheria za
Uingereza hazitakiwi kutumika kuamua katika kesi za uchaguzi, Mugwai
alidai Jaji Rwakibalila yupo sahihi kwani hata kifungu cha 1(2) cha
sheria ya uchaguzi sura ya 343, kinasema masuala yote ya uchaguzi
yatashughulikiwa kwa kutumia sheria ya uchaguzi na kuongeza kuwa
mawakili wa Lema wametumia kesi za Mahakama ya Rufaa zilizoamriwa kwa
sheria ya zamani ya uchaguzi ya mwaka 1985 wakati sheria hiyo ya
uchaguzi imeishafanyiwa marekebisho na marekebisho ya mwisho yalifanyika
mwaka 2010 .
“Hata kifungu cha 2 (3) cha sheria ya Judicuture and Application of
Law (JALA), inakataza matumuzi ya sheria za nje kutumika kuamua kesi za
uchaguzi wakati nchi yetu ina sheria mahususi ya uchaguzi kwa ajili ya
kuamua kesi za uchaguzi na kwamba jaji alikuwa sahihi kusema hilo na pia
alikuwa sahihi kusema wajibu rufaa walikuwa na haki ya kufungua kesi
hiyo na kuongeza kuwa hoja hiyo ni butu,” alidai wakili Mugwai.
Hata hivyo, alipinga hoja ya mawakili wa Lema iliyodai Jaji
Rwakibalila katika hukumu yake hakutumia kesi walizoziwasilisha mbele
yake, ambapo alidai katika hukumu hiyo alitumia baadhi ya kesi
walizoziwasilisha mbele yake na kwamba jaji ana mamlaka ya kuchuja kesi
anazotaka kuzitumia kwenye hukumu.
Akijibu hoja kwamba hukumu ya Lema iliegemea kwenye ushahidi wa
mazingira tu, wakili Mugwai alikanusha na kusema hakukuwepo ushahidi wa
mazingira kwani mashahidi waliomsikia Lema akitoa maneno ya kashfa
kwenye mikutano ya hadhara, walifika mahakamani hapo na kutoa ushahidi
wao ambapo walisema walimwona na kumsikia akfanya hivyo dhidi ya
Batilda.
Hata hivyo wakati wakili Mugwai akiwasilisha hoja zake, baadhi ya watu
wanaodaiwa ni wafuasi wa CHADEMA ambao walijazana ndani ya chumba cha
mahakama, waliguna na kutoa vicheko hali iliyosababisha wakili huyo
awaombe majaji wawadhibiti watu wenye tabia hiyo kwani mawakili wa Lema
walipokuwa wakiwasilisha hoja zao walitulia.
Rufaa hiyo inayovuta hisia za wengi ndani na nje ya nchi, ilianza
kusikilizwa majira ya saa tatu asubuhi na kumalizika saa tisa alasiri.
Kesi hiyo imeahirishwa na sasa kinachosubiriwa ni tarehe ya hukumu ili kukata mzizi wa fitina.
Kwa mujibu wa jopo hilo la majaji wa Mahakama ya Rufaa, tarehe ya
kutolewa uamuzi wa rufaa hiyo itatolewa kwa njia ya maandishi kwa
mawakili wa pande zote mbili.
|
No comments:
Post a Comment