|
MBUNGE wa Jimbo la Ubungo (CHADEMA), John Mnyika, jana
aliwasilisha katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam hoja binafsi
inayohusu uboreshaji wa huduma ya majisafi na uondoaji wa majitaka
katika maeneo mbalimbali jijini.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, iliyotumwa na Katibu
wa Mbunge Aziz Himbuka, alisema lengo la hoja hiyo ni kupendekeza baraza
la madiwani wa jiji, kujadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka
zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji
taka katika Jimbo la Ubungo na jiji katika masuala yaliyo chini ya
mamlaka ya halmashauri.
Mnyika alisema ameamua kuchukua hatua hiyo wakati huu ili Halmashauri
ya Jiji la Dar es Salaam iweze kutimiza wajibu wake mwezi huu, huku
akisubiri kuwasilisha hoja binafsi bungeni katika mkutano wa kumi
Februari 2013 endapo Wizara ya Maji haitachukua hatua zinazostahili.
Alisema pamoja na mafanikio ya kawaida yaliyopatikana kupitia mikutano
yake na wananchi katika kata mbalimbali jimboni kwake, ufuatiliaji
serikalini bado una matatizo yanayohitaji baraza la madiwani
kushughulikia kwa ajili ya Jimbo la Ubungo na Mkoa mzima wa Dar es
Salaam.
Mbunge huyo alisema kufuatilia masuala ya maji, alianza kwa kufanya
kongamano la Maji katika Jimbo
la Ubungo mwanzoni mwa mwaka 2011 ili kuwakutanisha wananchi, mamlaka
husika na wadau wengine katika kuunganisha nguvu kupata ufumbuzi.
Alizitaja hatua nyingine ambazo amekwishazichukua
ili ziweze kufanyiwa haraka ni pamoja na kuishirikisha DAWASA, DAWASCO
na Wizara ya Maji ambao alidai utekelezaji wao ulikuwa mdogo na kwamba
mpaka sasa hakuna ambacho kimeishafanyika.
Hivyo, Mnyika alisema kutokana na hilo aliamua kukusanya nguvu ya
pamoja kufanya maandamano ya kudai maji hadi katika ofisi kuu za
DAWASCO.
“Maandamano hayo yalizaa matunda kwa upande wa DAWASCO ambapo
ameshafanya nao ziara ya kikazi ya kata mbalimbali ya kutembelea maeneo
yenye matatizo na hatua zimechukuliwa ambazo zimewezesha baadhi ya
maeneo kuanza kutoka maji,” ilisema taarifa yake.
Hata hivyo alisema bado yapo maeneo mengi yenye matatizo makubwa ya maji ikiwemo ya Msumi,
Makabe, Msakuzi, Malambamawili, Msingwa, Goba na mengineyo mengi katika jiji la Dar es salaam.
|
No comments:
Post a Comment