|
MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA),
amesema Chama cha Mapinduzi (CCM) hakitaweza kufanikiwa kupambana na
kuzuia rushwa nchini, kutokana na viongozi wengi wa chama hicho
kupatikana kwa njia ya rushwa.
Msigwa aliyasema hayo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika viwanja vya Mwembetogwa mkoani hapa.
Mbali na Msigwa kuinyooshea kidole CCM kwa rushwa, Mkurugenzi wa
Kampeni na Uchaguzi CHADEMA, Msafiri Mtemelwa, alisema wakati wa Baba wa
Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, chama hicho tawala
hakikuwa kama kilivyo sasa.
Alisema CCM ilikuwa ina maadili mema, lakini hivi sasa kila kona
nchini imejaa rushwa ambayo inasababisha adha kubwa kwa maskini.
Aliongeza kuwa licha ya michakato mbalimbali ya kukibadili chama kwa
maana ya viongozi kama njia ya kukisafisha, wamekuwa wakisahau kuwa
wanaowapatia uongozi ni watu ambao tayari walishaiingiza nchi pabaya.
“Leo mmeambiwa viongozi wa CCM wamewabadilisha! Wamewabadilishieni
kanzu lakini mapadre au mashehe ni wale wale, Kinana ambaye aliaga siasa
basi anastaafu, leo amerudi kufuata nini?” alisema Mtemelwa.
Akitolea mfano kwa baadhi ya viongozi ambao wameipeleka nchi pabaya,
alimtaja aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula, akiwa na
mwenyekiti wake Benjamin Mkapa akidai kuwa walichangia kwa kiasi kikubwa
kuiyumbisha nchi.
“Mkapa na Mangula ndio walioifilisi nchi hii. Mangula aliuza nyumba za
serikali akiwa Katibu Mkuu na Mwenyekiti akiwa Mkapa. Mangula pia
aliuza machimbo ya almasi katika nchi hii yeye akiwa Katibu Mkuu na
Mwenyekiti akiwa Mkapa,” alisema.
Hata hivyo alidai kuwa Mwalimu Nyerere aliacha machimbo ya madini
maeneo mawili, Buhemba na Shinyanga Mwadui, lakini Rais Jakaya Kikwete
na wenzake wameuza North Mara Lyamungo pamoja na Buhemba mkoani Mara
huku wananchi wakiendelea kulia njaa.
Alieleza kuwa taifa la Tanzania ni taifa tajiri duniani kuliko sehemu
nyingine yoyote isipokuwa linakosa viongozi wenye maadili bora wa
kusimamia rasilimali hizo kwa manufaa ya taifa.
Aidha amewataka Watanzania hususan vijana kuchukua hatua za haraka za
kuchagua viongozi makini ili kuinusuru nchi kutoka mikononi mwa viongozi
wanaofanya kazi kwa maslahi binafsi na kuhakikisha Kikwete ndiye Rais
wa mwisho nchini kutoka CCM.
|
No comments:
Post a Comment