Friday, December 7, 2012

Wednesday, December 5, 2012

CCM haiwezi kupambana na rushwa – Msigwa






MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA), amesema Chama cha Mapinduzi (CCM) hakitaweza kufanikiwa kupambana na kuzuia rushwa nchini, kutokana na viongozi wengi wa chama hicho kupatikana kwa njia ya rushwa.
Msigwa aliyasema hayo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika viwanja vya Mwembetogwa mkoani hapa.
Mbali na Msigwa kuinyooshea kidole CCM kwa rushwa, Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi CHADEMA, Msafiri Mtemelwa, alisema wakati wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, chama hicho tawala hakikuwa kama kilivyo sasa.
Alisema CCM ilikuwa ina maadili mema, lakini hivi sasa kila kona nchini imejaa rushwa ambayo inasababisha adha kubwa kwa maskini.
Aliongeza kuwa licha ya michakato mbalimbali ya kukibadili chama kwa maana ya viongozi kama njia ya kukisafisha, wamekuwa wakisahau kuwa wanaowapatia uongozi ni watu ambao tayari walishaiingiza nchi pabaya.
“Leo mmeambiwa viongozi wa CCM wamewabadilisha! Wamewabadilishieni kanzu lakini mapadre au mashehe ni wale wale, Kinana ambaye aliaga siasa basi anastaafu, leo amerudi kufuata nini?” alisema Mtemelwa.
Akitolea mfano kwa baadhi ya viongozi ambao wameipeleka nchi pabaya, alimtaja aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula, akiwa na mwenyekiti wake Benjamin Mkapa akidai kuwa walichangia kwa kiasi kikubwa kuiyumbisha nchi.
“Mkapa na Mangula ndio walioifilisi nchi hii. Mangula aliuza nyumba za serikali akiwa Katibu Mkuu na Mwenyekiti akiwa Mkapa. Mangula pia aliuza machimbo ya almasi katika nchi hii yeye akiwa Katibu Mkuu na Mwenyekiti akiwa Mkapa,” alisema.
Hata hivyo alidai kuwa Mwalimu Nyerere aliacha machimbo ya madini maeneo mawili, Buhemba na Shinyanga Mwadui, lakini Rais Jakaya Kikwete na wenzake wameuza North Mara Lyamungo pamoja na Buhemba mkoani Mara huku wananchi wakiendelea kulia njaa.
Alieleza kuwa taifa la Tanzania ni taifa tajiri duniani kuliko sehemu nyingine yoyote isipokuwa linakosa viongozi wenye maadili bora wa kusimamia rasilimali hizo kwa manufaa ya taifa.
Aidha amewataka Watanzania hususan vijana kuchukua hatua za haraka za kuchagua viongozi makini ili kuinusuru nchi kutoka mikononi mwa viongozi wanaofanya kazi kwa maslahi binafsi na kuhakikisha Kikwete ndiye Rais wa mwisho nchini kutoka CCM.

Mnyika apeleka hoja ya maji Halmashauri


MBUNGE wa Jimbo la Ubungo (CHADEMA), John Mnyika, jana aliwasilisha katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam hoja binafsi inayohusu uboreshaji wa huduma ya majisafi na uondoaji wa majitaka katika maeneo mbalimbali jijini.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, iliyotumwa na Katibu wa Mbunge Aziz Himbuka, alisema lengo la hoja hiyo ni kupendekeza baraza la madiwani wa jiji, kujadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jimbo la Ubungo na jiji katika masuala yaliyo chini ya mamlaka ya halmashauri.
Mnyika alisema ameamua kuchukua hatua hiyo wakati huu ili Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iweze kutimiza wajibu wake mwezi huu, huku akisubiri kuwasilisha hoja binafsi bungeni katika mkutano wa kumi Februari 2013 endapo Wizara ya Maji haitachukua hatua zinazostahili.
Alisema pamoja na mafanikio ya kawaida yaliyopatikana kupitia mikutano yake na wananchi katika kata mbalimbali jimboni kwake, ufuatiliaji serikalini bado una matatizo yanayohitaji baraza la madiwani kushughulikia kwa ajili ya Jimbo la Ubungo na Mkoa mzima wa Dar es Salaam.
Mbunge huyo alisema kufuatilia masuala ya maji, alianza kwa kufanya kongamano la Maji katika Jimbo la Ubungo mwanzoni mwa mwaka 2011 ili kuwakutanisha wananchi, mamlaka husika na wadau wengine katika kuunganisha nguvu kupata ufumbuzi.
Alizitaja hatua nyingine ambazo amekwishazichukua ili ziweze kufanyiwa haraka ni pamoja na kuishirikisha DAWASA, DAWASCO na Wizara ya Maji ambao alidai utekelezaji wao ulikuwa mdogo na kwamba mpaka sasa hakuna ambacho kimeishafanyika.
Hivyo, Mnyika alisema kutokana na hilo aliamua kukusanya nguvu ya pamoja kufanya maandamano ya kudai maji hadi katika ofisi kuu za DAWASCO.
“Maandamano hayo yalizaa matunda kwa upande wa DAWASCO ambapo ameshafanya nao ziara ya kikazi ya kata mbalimbali ya kutembelea maeneo yenye matatizo na hatua zimechukuliwa ambazo zimewezesha baadhi ya maeneo kuanza kutoka maji,” ilisema taarifa yake.
Hata hivyo alisema bado yapo maeneo mengi yenye matatizo makubwa ya maji ikiwemo ya Msumi, Makabe, Msakuzi, Malambamawili, Msingwa, Goba na mengineyo mengi katika jiji la Dar es salaam.

Petroli bei juu






MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo ya bidhaa za mafuta ya petroli nchini ambayo imeongezeka kwa sh 70 kwa lita sawa na asilimia 3.4.
Hatua hiyo ni wazi kuwa itasababisha gharama za nauli kuwa juu, pamoja na usumbufu kwa abiria katika nyakati hizi za kuelekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Anastas Mbalawa kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Haruna Masebu, alisema kuwa bei hizo zitaanza kutumika kuanzia leo na kuwataka wamiliki wa vituo vya mafuta kutambua bei kikomo ya bidhaa hizo.
Taarifa hiyo ilitaja bei hizo katika Jiji la Dar es Salaam kwa petroli itakuwa sh 2,119, dizeli sh 1,999 na mafuta ya taa sh 2,023; Arusha petroli sh 2,203, dizeli sh 2,083 na mafuta ya taa sh 2,107 huku Dodoma petroli itauzwa sh 2,146, dizeli sh 2,058 na mafuta ya taa sh 2,082.
Mkoani Iringa petroli itauzwa kwa sh 2,183, dizeli sh 2,063 na mafuta ya taa sh 2,087, huku Morogoro petroli itauzwa kwa sh 2,144, dizeli sh 2,024 na mafuta ya taa sh 2,048 na Bukoba petroli sh 2,334, dizeli sh 2,214 na mafuta ya taa sh 2,238.
Alisema kuwa bei za jumla na rejareja kwa mafuta aina zote ya petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka ikilinganishwa na toleo lililopita la Novemba 7, 2012.
“Katika toleo hili, bei za rejareja kwa dizeli imeongezeka sh 10 kwa lita sawa na asilimia 0.53, bei ya mafuta ya taa imepungua kwa sh 3 kwa lita sawa na asilimia 0.1, huku bei za jumla kwa kulinganisha matoleo haya mawili zimeongezeka petroli kwa sh 69.56 kwa lita sawa na asilimia 3.52; dizeli kwa sh 10.04 kwa lita sawa na asilimia 0.52,” alisema.
Alisema kuwa bei ya mafuta ya taa imepungua kwa sh 3 kwa lita sawa na asilimia 0.15 huku akisema kuwa mabadiliko ya bei hizo yametokana na ongezeko la bei ya mafuta katika soko la dunia na kushuka kidogo kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani.
Mbalawa alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko ambapo EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa hizo.
“Kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo (price cap) kama ilivyokokotolewa na fomula mpya iliyopitishwa na mamlaka yetu na kuchapwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 454 la Desemba 23, 2011,” alisema.
Aidha, alisema kuwa ni muhimu vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa hizo katika mabango yanayoonekana, huku ikionyesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika.
Alisema kuwa ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja, na kwamba adhabu itatolewa kwa kituo husika.

Dk. Slaa, Nape jino kwa jino






KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amesema anampongeza Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa, kwa kukiri kwamba anamiliki kadi ya CCM hadi leo.
“Kwanza nampongeza kwa kuanza kujifunza kusema ukweli maishani mwake, bila shaka ametambua kuwa uongo haulipi. Kitendo cha kukiri anamiliki kadi ya CCM bado ni cha kiungwana, nampongeza kwa hili,” alisema Nape, baada ya mwandishi wetu kumtaka maoni yake juu ya Dk. Slaa kukiri kumiliki kadi ya CCM hadi sasa.
Akijibu tuhuma za Nape alizotoa juzi kwamba baadhi ya vigogo wa CHADEMA akiwemo Dk. Slaa, bado wana kadi za CCM na baadhi yao wanaendelea kuzilipia, Katibu huyo wa CHADEMA kupitia vyombo vya habari, amekiri kuwa anayo kadi ya CCM na kwamba anaitunza kama kumbukumbu muhimu kwake.
Pia Dk. Slaa alisema Nape anapiga mayowe na kumtaka asiwapotezee muda Watanzania kwa kujadili mambo yasiyo na msingi na kuacha kujadili suala la umaskini na jinsi ya kuwasaidia kuondokana na hali hiyo.
Pamoja na pongezi hizo, Nape amemtaka Dk. Slaa kuwaambia Watanzania kwamba kadi hiyo ameilipia mpaka lini, pia aache tabia ya kuwadanganya wenzake kurudisha kadi zao za CCM huku yeye akibaki na yake kibindoni.
“Ni vizuri sasa Dk. Slaa awaambie Watanzania amelipia mpaka lini kadi hii. Lakini aache kuwadanganya wenzake kurudisha kadi zao huku yeye akibaki na yake huu ni unafiki,” alisema Nape.
Aidha Nape ambaye amekiri kumheshimu sana Dk. Slaa kama Babu yake, amesema alishtuka sana kusikia Katibu Mkuu huyo wa CHADEMA akiwatuhumu viongozi wa chama hicho, hivi karibuni kuwa ni mamluki wa CCM huku akijua yeye ni mamluki namba moja kwani wenzie hawana kadi za CCM yeye anayo.
“Nimesikia anahoji hili linawasaidiaje Watanzania maskini! Swali hili limethibitisha upeo mdogo sana wa kufikiri wa kiongozi mkubwa na ninayemheshimu kama huyu. Lazima ajue kwamba yeye anaomba kuwa kiongozi, hivyo lazima wananchi tumjue tabia zake,” alisema Nape na kuongeza:
“Viongozi wanafiki wa aina yake ni janga kwa taifa letu.Usipokuwa mwaminifu kwa kidogo huwezi kuwa mwaminifu kwa kikubwa. Lazima anayetaka kuwa kiongozi aishi anayoyasema.”